• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
36 kuhojiwa kujaza nafasi 4 za makamishna IEBC

36 kuhojiwa kujaza nafasi 4 za makamishna IEBC

Na LEONARD ONYANGO

MAHOJIANO ya kutafuta watakaochua nafasi nne za makamishna katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) yataanza Juni 30 huku watu 36 kati ya 660 waliotuma maombi, wakiorodheshwa kushiriki.

Maombi ya watu 624 waliotaka kujiunga na tume hiyo yalikataliwa na kamati maalumu ya kuteua makamishna wa IEBC inayoongozwa na Dkt Elizabeth Muli.Miongoni mwa waliotuma maombi ya kutaka kuwa kamishna wa IEBC ni kijana wa umri wa miaka 23 huku mtu wa umri wa juu zaidi alikuwa na miaka 73.

Walioorodheshwa watafanyiwa mtihani wa kisaikolojia katika jumba la KICC jijini Nairobi Juni 30.Mahojiano ya mazungumzo yataanza Julai 7 hadi Julai 22 na watu watatu watahojiwa kwa siku.Nafasi hizo zilisalia wazi kufuatia kujiuzulu kwa waliokuwa makamishna Roselyn Akombe, Paul Kurgat, Margaret Mwanchanya na Connie Maina baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Kamati hilo imewataka Wakenya kuwasilisha taarifa za kupinga au kuunga mkono watu hao 36 ili kuiwezesha kufanya uamuzi wa busara.

Siku ya mwisho ya kuwasilisha taarifa hizo ni Juni 25.Miongoni mwa watakaohojiwa ni aliyekuwa mbunge wa Gwassi (sasa Suba Kusini) Felix Nyauchi, aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Huduma kwa Polisi (PSC) Abdalla Mohamed (Nairobi), aliyekuwa naibu mwenyekiti wa bodi ya kuchunguza maadili ya majaji na mahakimu Roseline Adhiambo Odede (Siaya) na aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa kuhusu Haki za Kibinadamu (KNCHR) Kagwigira Mbogori (Meru).

Dkt Catherine Muchiru Kamindo, kaimu mkurugenzi wa utafiti na mipaka wa IEBC pia atahojiwa pamoja na mwenzake Paloshe Tobiko, ambaye ni meneja wa huduma katika tume hiyo. Aliyekuwa mkurugenzi wa wafanyakazi wa IEBC Sellestine Kiuluku pia ni miongoni mwa walioorodheshwa.

Mawakili walio katika orodha hiyo ni Bw Nyauchi, aliyekuwa naibu wa rais wa Chama cha Wanasheria Harriette Chiggai, Justus Munyithya na Bi Odede.Makamishna hao wanatarajiwa kusimamia uchaguzi wenye ushindani mkubwa baadaye mwaka ujao.

  • Tags

You can share this post!

Chipu yapasua Mwamba raga ya kujiandalia Kombe la Afrika

Muungano wa kisiasa wa kaunti za Mashariki pigo kwa Mlima...