• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Ajipata kizimbani kwa madai ya kuiba nakala mbili za Biblia

Ajipata kizimbani kwa madai ya kuiba nakala mbili za Biblia

Na RICHARD MUNGUTI

KIBARUA aliyeiba nakala mbili za Biblia kutoka dukakuu asome aimarishe maisha yake ya kiroho, Jumatano alifikishwa mahakamani Milimani.

Augustine Wanyonyi aliyeshtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi Wandia Nyamu alikanusha shtaka la kuiba kitabu hiki kitakatifu.

Bi Nyamu alifahamishwa na kiongozi wa mashtaka kuwa Wanyonyi alikamatwa na mabawabu katika dukakuu la Naivas lililoko barabara ya Moi Avenue jijini Nairobi.

Wanyonyi aliyekuwa akijibu shtaka aliomba aachiliwe kwa dhamana.

Lakini ombi hilo lilipingwa vikali na kiongozi wa mashtaka akisema: “Wanyonyi alikataa alama za vidole zikichukuliwa ili ibainike iwapo amewahi kushiriki katika uhalifu hapo awali.”

Kutokana na hatua hiyo, hakimu aliamuru mshtakiwa apelekwe katika kituo cha polisi cha Central kuchukuliwa alama za vidole.

Mahakama ilielezwa kuwa alizua kioja ndani ya kituo cha polisi alipokataa kuchukuliwa alama za vidole.

Hakimu aliamuru Wanyonyi aliyekana kuiba nakala mbili za Biblia zenye thamani ya Sh1,800 mnamo Novemba 29, 2021 kurudishwa kortini jana Alhamisi kwa maagizo zaidi.

You can share this post!

Mzee aenda kortini kudai pesa kutoka kwa mwanawe

Corona yafagia asilimia 35 ya biashara ndogo

T L