• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Amri Balala, Keter wafike mbele ya Seneti

Amri Balala, Keter wafike mbele ya Seneti

Na ERIC MATARA

SENETI imewaagiza mawaziri Najib Balala (Utalii) na Charles Keter (Kawi) kufika mbele yake, kufuatia kisa cha wikendi iliyopita ambapo twiga watatu walifariki baada ya kupigwa na stima katika Shamba la Soysambu, Kaunti ya Nakuru.

Spika wa Seneti, Bw Kenneth Lusaka aliwaagiza wawili hao kufika mbele ya Seneti wiki ijayo, baada ya Seneta George Khaniri wa Vihiga, kutaka maelezo kuhusu kilichosababisha tukio hilo.

“Ninawaagiza mawaziri wa Utalii na Kawi mtawalia kufika mbele ya Seneti na kuelezea hali iliyosababisha mkasa huo, ambapo twiga aina ya Rothchild’s walifariki,” akasema.

Kisa hicho kimesababisha hisia kali kutoka kwa viongozi na wanaharakati wa uhifadhi wa wanyama.

“Utakuwa mfano mbaya ikiwa hakuna yeyote atakayeadhibiwa kutokana na kutowajibika huko. Zaidi ya hayo, wizara zote husika zinapaswa kufanya tathmini ya pamoja kuhusu hali ya usalama katika mashamba yote ya kuwahifadhi wanyamapori nchini,” akasema Bw Khaniri.

Maseneta Johnson Sakaja (Nairobi) na Mutula Kilonzo Junior (Makueni) pia waliomba maelezo kuhusu kisa hicho.

“Twiga aina ya Rothchild ni 1,600 pekee kote duniani na karibu robo moja kote nchini. Hatuwezi kuruhusu utepetevu kama huu kuendelea,” akasema Bw Sakaja.

Seneta Aaron Cheruiyot (Kericho) pia alimtaka Bw Balala kelezea kuhusu kisa ambapo vifaru 10 walifariki katika hali tatanishi mnamo 2018.

Wanyama hao walikuwa miongoni mwa vifaru 14 waliokuwa wakisafirishwa kutoka Mbuga ya Wanyama ya Nairobi hadi katika Mbuga ya Wanyama ya Tsavo, iliyo katika Kaunti ya Taita Taveta.

Hisia hizo zinajiri hata baada ya Kampuni ya Kusambaza Umeme Kenya Power kuomba radhi wiki hii.

Vuguvugu la Kutoa Hamasisho kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa (CCAK) pia limeitaka serikali ihakikishe mazingira yote ya wanyamapori yamelindwa.

Vilevile, linataka hatua kali kuchukuliwa ili kuhakikisha mazingira hayo hayawekwi nyua zinazowazuia wanyamapori kutembea watakavyo.

Lilisema linamtaka Bw Balala kujiuzulu kuhusiana na kisa hicho.

You can share this post!

Kichwa kinauma

Kampeni za Matungu zaingia hatua ya lala-salama