• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 12:41 PM
Ashtakiwa kwa kutaka kulamba kifua cha polisi

Ashtakiwa kwa kutaka kulamba kifua cha polisi

NA JOSEPH NDUNDA

MWANAMUME mmoja mwenye umri wa miaka 29 aliyejaribu kufikia kifua cha afisa wa polisi wa kike aliyekuwa akimkamata katika nyumba yake katika mtaa wa mabanda wa Fuata Nyayo jijini Nairobi ameshtakiwa kwa kufanya kitendo cha aibu kinachokiuka sehemu ya 11 (1) ya Sheria ya Makosa yanayohusiana na Ngono ya 2006.

Ben Marita Mokema almaarufu Jembe Kali alishtakiwa kwa kufanya nakusudi kitendo kilicho kinyume cha kisheria cha  kulamba sehemu ya kifua cha polisi mwanamke bila idhini yake mnamo Julai 21, 2023.

Mshukiwa aliyekuwa akichechemea akipandishwa kizimbani alikanusha mashtaka mbele ya Hakimu Mwandamizi Irene Gichobi katika Mahakama ya Makadara, akisema alikuwa amelewa wakati wa kitendo hicho.

Afisa mlalamishi na wenzake wawili kutoka Mariguini tarafa ya South B walikuwa wameenda kumkamata Mokema baada ya mwanamke kumripoti kwamba alikuwa amembaka katika nyumba yake.

Polisi walibisha kwa mlango mara kadhaa lakini Mokema alidinda kuufungua. Alichungulia kwa dirisha kisha akazima taa alipowaona maafisa kwa mlango.

Alipoambiwa amkabidhi mwanamke aliyedai kubakwa, laputopu yake, mwanamume huyo alisisitiza ni mpenzi wake.

Hata hivyo alifungua mlango akarusha laputopu nje lakini kabla afunge mlango, polisi walijitoma ndani na wakamwambia walikuwa wamemtia mbaroni. Walimweleza sababu ya kumkamata lakini akazua vurugu.

Alijaribu kutwaa kisu lakini akapokonywa na baadaye akajaribu kumlamba ‘kifua’.

Anakabiliwa pia na kosa la kumshambulia polisi na kumzuia kufanya kazi.

Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh60,000 na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho bila kuruhusiwa dhamana ya pesa taslimu.

Kesi itatajwa mnamo Agosti 16 na kuanza kusikilizwa mnamo Septemba 25, 2023.

Mlalamishi na polisi wengine wawili, pamoja na daktari aliyemtibu wameorodheshwa kama mashahidi dhidi ya Mokema.

Jumanne wiki jana Mokema alikabiliwa na shtaka la ubakaji alilokanusha mbele ya Hakimu Mkuu Francis Kyambia na akazuiliwa katika Gereza la Industrial Area kusubiri kukabiliwa na mashtaka ya jana Jumanne.

  • Tags

You can share this post!

Ruto ainua nyaunyo kuchapa wazembe

Mzaha mzaha huzaa talanta

T L