• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:02 PM
Askofu apongeza serikali kwa kufunga baa za kero tele katika eneo la Kahawa Wendani

Askofu apongeza serikali kwa kufunga baa za kero tele katika eneo la Kahawa Wendani

NA LAWRENCE ONGARO

SERIKALI imepongezwa kwa kuchukua hatua kali ya kufunga baadhi ya maskani ya burudani jijini Nairobi na vitongoji vyake.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Glory Outreach Assembly (GOA) eneo la Kahawa Wendani, David Munyiri Thagana, ameipongeza serikali kwa kuchukua hatua hiyo haraka ipasavyo.

“Kwa muda mrefu maskani za burudani zimekuwa kero kwa Wakenya wengi hasa wanaoishi karibu na maeneo hayo. Wengi ambao wameathirika sana ni wanafunzi wa shule,” alifafanua mchungaji huyo.

Alisema baa za kuuza pombe zilizo karibu na makazi ya watu ni kero kubwa kwa wananchi.

Vile vile alisema uwepo wa baa hizo husababisha msongamano wa magari katika maeneo hayo.

“Sisi kama wachungaji tunataka serikali kushikilia msimamo huo kwa sababu familia nyingi zinazoishi karibu na maskani hizo za kuuza pombe hawana amani kabisa,” alieleza Askofu Thagana.

Kulingana naye, maeneo yaliyoathirika sana ni Bypass na Kahawa Wendani.

“Usiku kucha walevi hubugia pombe huku muziki ukipigwa kwa sauti ya juu hali familia nyingi zinazoishi karibu na hapo wakikosa usingizi. Kwa hivyo, serikali iendelee kuchukua hatua hiyo ya kufunga maeneo hayo,” alifafanua mchungaji huyo.

Alisema serikali inastahili kuingilia kati haraka ili kuokoa vijana ambao pia wameingilia unywaji wa pombe kiholeka bila kujali maisha yao ya baadaye wanakuwa kwa mkondo mwema.

Alisema hata ingawa biashara hiyo inainua uchumi wa nchi, ukweli wa mambo ni kwamba walevi wengi huathirika kiakili huku wakistahili kutafuta matibabu ya kiafya.

Alisema vijana wengi wameingilia utumizi wa dawa za kulevya na pombe kwa kishindo na kwa hivyo ni vyema wakipatiwa mwelekeo wa kimaisha.

“Ili wananchi waweze kupata maisha mazuri serikali isilegeze kamba bali izidi kukabiliana vilivyo na wale wanaozidi kuendeleza maskani za burudani,” akasema na kuahidi wachungaji wataendelea kuiombea nchi ya Kenya ili wananchi wazidi kuishi kwa amani.

Alisema ni hivi majuzi taifa limetoka kwa uchaguzi na kwa hivyo nchi inastahili kuwa na mshikamano bila kujali ni mirengo gani ya kisiasa mtu anashabikia.
  • Tags

You can share this post!

Borussia Dortmund watoka nyuma na kulazimishia Bayern...

IMLU yatoa takwimu kuhusu mauaji ya kiholela nchini

T L