• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:07 PM
Azimio sasa washtaki serikali kuhusu mauaji ya walioandamana kulalamikia ugumu wa maisha

Azimio sasa washtaki serikali kuhusu mauaji ya walioandamana kulalamikia ugumu wa maisha

Na SAM KIPLAGAT

MUUNGANO wa Azimio la Umoja One Kenya umewasilisha ombi mahakamani kutaka familia za watu 75 wanaodaiwa kuuawa na polisi wakati wa maandamano walipwe fidia.

Muungano huo ulisema katika ombi hilo kwamba afisa yeyote wa polisi aliyekuwa akisimamia kitengo maalum wakati wa maandamano alikiuka sheria na anapaswa kuwajibika.

Kupitia kwa wakili Paul Mwangi, muungano huo ulisema wakuu wa polisi wanapaswa kubeba lawama kwa sababu ama waliamuru matumizi ya nguvu kupita kiasi au kujifanya kutofahamu yaliyotokea wakati wa maandamano.

“Ombi hilo linalenga kuzisaidia familia za watu 75 walioaga dunia na kwa watu wengine walioaga dunia au kujeruhiwa, ambao walikuwa waathiriwa wa ukatili wa polisi katika kipindi hicho,” ombi hilo lililowasilishwa na wakili Paul Mwangi lilisema.

Ombi hilo linaitaka mahakama itoe amri kwamba maafisa waliotenda ukatili huo wachukuliwe hatua.

Kando na fidia kwa waathiriwa, muungano wa upinzani unaitaka mahakama kushurutisha mashirika ya serikali kuchunguza na kufanya uchunguzi kuhusu vitendo vya maafisa wa polisi.

Wakili huyo alisema polisi wanafungwa na kanuni ya jumla ya sheria ya kimataifa ya uwajibikaji na wanapaswa kuwajibika kwa hatua zilizosababisha vifo vya watu 75.

“Watu sabini na watano waliokufa walikuwa wakiandamana kama ilivyoainishwa kwenye katiba.”

Ombi hilo lilisema Inspekta Jenerali wa Polisi Japet Koome anafaa kuzingatia sheria na kulinda haki za binadamu na uhuru wa kimsingi.

Zaidi ya hayo, kwamba haikuwa sahihi kwa mkuu wa polisi kupiga marufuku maandamano hayo, hatua ambayo ombi hilo linasema ilikiuka sheria inayowapa watu nafasi ya kuandamana.

Ombi hilo liliongeza kuwa polisi walitumia nguvu kupita kiasi jambo lililosababisha vifo vya watu 75.

“Mlalamishi anasisitiza kwamba kanuni ya jumla ya sheria ya kimataifa ya wajibu wa amri inahusisha wajibu wa kuelimisha, kusimamia, kuzuia, kuchunguza na kuadhibu walio chini yake,” Bw Mwangi alisema.

Bw Mwangi alisema mkuu wa polisi alikuwa ametoa taarifa ya kupiga marufuku maandamano yote nchini na hata kutowachukulia hatua polisi waliokuwa wakivuruga maandamano hayo ya amani.

  • Tags

You can share this post!

DOMOKAYA: Lejendari Kipchoge hakika hajaonyesha picha nzuri...

Mpenzi ana tabia ya kumezea mate visura waziwazi na...

T L