• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Baadhi ya wanawake ambao magenge ya uhalifu Maragua yameua

Baadhi ya wanawake ambao magenge ya uhalifu Maragua yameua

NA MWANGI MUIRURI

MJI wa Maragua ulio katika Kaunti ya Murang’a umejipa sifa mbaya ya kuwa ngome ya magenge ya uhalifu ambayo yakiwa chini ya msukumo wa mihadarati na vileo vya mauti, hutwika jamii maombolezi si haba.

Walioumia zaidi katika ujambazi huu ni wanawake ambao kwa unyonge wao, wamejipata hoi mikononi mwa wahuni, baadhi yao wakijipata wakipoteza maisha.

Orodha ifuatayo ni baadhi ya wanawake ambao wamejipata ndani ya jeneza kutokana na uhalifu wa mji huu na viunga vyake.

Wanjiku wa Njambi, 28

Mnamo Agosti 19, 2023 aliuawa na mshukiwa wa uuzaji bhangi ambaye alikuwa akiishi naye kama mume na mke.

Ripoti ya upasuaji ilionyesha kuwa alipewa kichapo cha mbwa na hatimaye akanyongwa.

Wanjiku wa Njambi, 28

Mwanamume huyo akitambulika kama David Kariuki alijaribu kujipeleka wake katika Mochari ya Maragua, wahudumu wakakataa kuupokea lakini polisi wa kituo cha Maragua wakampa idhini ya kujipelekea hadi mochari ya Murang’a.

Baada ya raia kuzusha, Bw Kariuki alikamatwa na kwa sasa anawajibikia kesi.

Catherine Njeri, 34

Aprili 2, 2023 Bi Njeri alipata shida ya kupumua na akaaga dunia alipokuwa akikimbizwa katika hospitali ya Maragua kupata matibabu.

Alikuwa ameandikisha taarifa katika kituo cha polisi cha Maragua mnamo Novemba 8, 2022 kwamba kuna mwanamume aliyekuwa akimtishia maisha.

Catherine Njeri, 34

Mwanamume huyo alikuwa akiishi naye kama mkewe, lakini akiwa mshukiwa wa ujambazi, alikuwa akimdhulumu mara kwa mara.

Baada ya maafisa hao kudinda kumtia mbaroni, Bi Njeri aliishia kuuawa.

Mercy Njoya

Januari 24, 2022 Bi Mercy Njoya alivamiwa nyumbani kwake katika mtaa wa Mathare na genge la vijana watatu ambao walimlipua kwa kutumia bomu la petroli.

Vijana hao walikuwa wameonekana katika baa moja inayojulikana kama Coro, wakibugia pombe mwendo wa saa nane usiku.

Inasemwa kwamba walimfuata Bi Njoya hadi nyumbani kwake na baada ya kuvunja mlango, wakamrushia bomu la petroli na aliaga dunia siku 13 baadaye akiwa katika hospitali kuu ya Kenyatta.

Purity Njeri Chege, 8

Julai 18, 2020 mtoto Purity Njeri alipatikana ameuawa na mwili wake kuwekwa kwenye gunia na kuzikwa katika kijiji cha Ihiga-ini.

Mshukiwa mkuu wa mauaji hayo ni kijana wa miaka 15 na baada ya kukamatwa, aliishia kuripotiwa kutoweka kimiujiza kutoka jela la watoto la Murang’a.

Purity Njeri, 8

Bw John Chege ambaye ni babake Njeri, kwa sasa huishi na mahangaiko kwa niaba ya familia yake kwa kukosa haki dhidi ya mauti hayo.

Kesi ya kusaka haki ya Bi Njeri imekwama katika mahakama kuu ya Murang’a huku kwa miaka mitatu sasa, idara ya uchunguzi wa makosa ya jinai (DCI) ikionyesha uzembe wa hali ya juu kumsaka mshukiwa huyo ambaye huonekana katika miji ya Nyahururu na Lamu kwa watu wa ukoo wao.

Charity Njeri Kimathi

Novemba 4, 2021 mchuuzi huyu wa maziwa katika mji wa Maragua alipatikana ameuawa.

Mwajiriwa wake wa kiume alikamatwa na maafisa wa polisi baada ya kunaswa akiwa na simu ya marehemu.

Charity Njeri Kimathi

Mshukiwa huyo aliorodheshwa kama mtumizi wa mihadarati, na kwa sasa anawajibikia kesi yake kortini.

Judy Wanjiru Gacheru, 32

Oktoba 15, 2018 Bi Judy Wanjiru alipatikana katika chumba cha mshukiwa aliyekuwa rafiki yake wa kimapenzi.

Tukio hilo la kijiji cha Kambirwa liliwaacha wenyeji vinywa wazi kwa kuwa mshukiwa alimtwanga nyundo ya kitovu cha kichwa na kisha akamkata shingo na kumweka kwa kitanda huku damu ikitiririka kwa karai.

Mwanamume huyo alikuwa ameripoti mara kadha katika kituo cha polisi cha Maragua akiwataka maafisa wamsaidie kupata pesa zake alizokuwa akidai kuibiwa na mwanamke huyo wa kuuza baa mjini humo.

Judy Wanjiru Gacheru, 32

Lakini baada ya kukosa usaidizi, inaaminika alichukua sheria mikononi na akamwangamiza Bi Wanjiru.

Baada ya kukosa hamu ya kumkamata, presha ya kampuni ya Nation Media Group ambayo huchapisha gazeti la Taifa Leo miongoni mwa mengine, iliangazia kisa hicho na akaishia kukamatwa 2022 na kwa sasa anajitetea kortini.

Ruth Njeri Mbau

Ilikuwa ni Novemba 24, 2018 mwendo wa saa tatu usiku ambapo mwanadada huyu alipatikana ameuawa kwa kukatwa shingo nje ya kituo cha polisi cha Maragua.

Ni kisa kilichoonyesha dharau kuu kwa maafisa wa kituo hicho kwamba mvamizi angemvizia mwathiriwa nje ya kituo cha polisi na amkate shingo.

Mshukiwa huyo alinaswa siku iliyofuata akiwa mbioni kuhepa lakini kwa sasa anajitetea kortini.

Jane Nduta Murage

Mnamo Januari 26, 2017 Bi Nduta alitoka baa ya Joyland iliyoko katika eneo la Kaharate akielekea nyumbani Maragua, alikokuwa amekodisha nyumba.

Hata hivyo, inaaminika kwamba alikumbana na genge moja hatari la Maragua lililomnajisi na kumpiga hadi akapata majeraha mabaya yaliyomuua siku 10 baadaye akitibiwa katika hospitali ya Outspan iliyoko Nyeri.

Mji huu umekuwa ukisumbuliwa na magenge haya ambayo hata hunajisi watoto wachanga.

Naibu Kamishna Bw Gitonga Murungi anasema kwamba “tumekuwa tukijibu mipigo ya kimikakati na kwa sasa licha ya changamoto, tumeimarisha hali”.

Bw Murungi anasema kwamba polisi wana maagizo imara kwamba kusiwe na kubembeleza washukiwa wa uhalifu na kwa mujibu wa sheria, hata wa kupigwa risasi apigwe.

Hayo yakijiri, hata wachuuzi wa kike hujipata mara kwa mara wametekwa nyara na kuibiwa pesa zao na magenge ambayo hata huwa yamejihami kwa bunduki.

 

[email protected]

 

 

  • Tags

You can share this post!

Simba apokonya mtalii kamera na kujirekodi ‘selfie’

Serikali kuondoa visa kwa Waafrika wanaozuru Kenya

T L