• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Bakora ya serikali sasa yaangukia bodaboda

Bakora ya serikali sasa yaangukia bodaboda

NA WANDERI KAMAU

WAHUDUMU wa bodaboda sasa watatozwa faini kali kwa kiukiuka sheria za trafiki au kubeba mizigo kupita kiasi, ikiwa Seneti itapitisha mswada uliowasilishwa na Kiranja wa Wengi katika Seneti, ambaye pia ni seneta wa Kakamegam Boni Khalwale.

Na sasa, Serikali inaonekana kuelekeza ‘mjeledi’ wake wa kuwatoza ushuru raia kwa wahudumu wa bodaboda, baada ya kuanza kuwatoza Wakenya wengine aina tofauti za ushuru, kama vile makato ya hazina ya nyumba.

Kulingana na mapendekezo ya Mswada wa Sheria ya Usafiri wa Umma (Kanuni za Pikipiki), 2023, ambao tayari umewasilishwa Seneti, hakuna mhudumu yeyoye wa bodaboda atakayeruhusiwa kumbeba zaidi ya abiria mmoja barabarani kwa wakati wowote ule.

Atakakayepatikana akikiuka kanuni hiyo atatozwa jumla ya Sh20,000, kufungwa gerezani kwa miezi sita au kukabiliwa na adhabu zote mbili.

Pendekezo jingine ni kuwa, mhudumu yeyote wa bodaboda atakayepatikana akiendesha pikipiki yake katika njia zilizotengewa watembeao kwa miguu au akiendesha pikipiki yake upande wa pili wa barabara, atatozwa faini ya Sh20,000, kifungo cha miezi sita gerezani au kukabiliwa na adhabu zote mbili.

Mswada huo pia unapendekeza adhabu kali dhidi ya wahudumu wanaowashambulia wenzao au waendeshaji magari. Wahudumu watakaopatikana wakiwashambulia wenzao watatozwa faini ya Sh100,000 , kifungo cha mwaka mmoja gerezani au kukabiliwa na adhabu zote mbili.

Unaeleza mswada: “Mtu yeyote atakayekiuka sehemu yoyote ya Sheria hii na faini yake haijaelezwa kwenye sheria hii akakuwa amefanya kosa na anafaa kushtakiwa na kupigwa faini ya Sh20,000, kufungwa gerezani kwa miezi sita au kukabiliwa na adhabu zote mbili.”

Mswada pia unawataka wauzaji pikipiki nchini kuuza pikipiki ikiwa na kofia mbili na jaketi mbili zinazotimiza masharti yaliyowekwa na Halmashauri ya Kukadiria Ubora wa Bidhaa Kenya (KEBS).

Chini ya mswada huo, wahudumu watazuiwa kubeba vifaa ama bidhaa haramu.

Abiria watakaopatikana wakibebwa na bodaboda bila kuvaa kofia au jaketi pia wataadhibiwa.

Chini ya mapendekezo hayo, abiria hawataruhusiwa kubebwa na pikipiki iliyobeba mzigo uliozidi kilo 50.

Pikipiki pia zitatarajiwa kutobeba mzigo ambao upana wake una ukubwa wa sentimita 15 zaidi ya mpini wake au ambao urefu wake ni zaidi ya mita mbili kutoka chini.

Pia, unaeleza kuwa yeyote anayemiliki pikipiki kwa matumizi ya kibiashara lazima ajisajilishe kwa chama cha ushirika, kama inavyohitajika na Sheria ya Vyama vya Ushirika. Kinaya ni kuwa, wahudumu wengi wa bodaboda nchini hawajajisajilisha kwa vyama vyovyote maalum vya ushirika.

Mapendekezo mengine ni kuwa: Mwanabodaboda hataruhusiwa kumbeba mtu anayepanga kujiingiza katika uhalifu, hataruhusiwa kuendesha pikipiki upande wa pili wa barabara na hataruhusiwa kuendesha pikikipi yenye mjazo wa injini usiozidi 250cc.

Wahudumu wa Tuktuk pia hawajasazwa kwenye masharti hayo mapya, kwani watahitajika tu kuwabeba abiria watatu pekee.
Mswada pia unaeleza kuwa wahudumu wa tuktuk hawataruhusiwa kuendesha tuktuk yenye ujazo wa injini unaopita 200cc katika barabara ya umma bila idhini rasmi ya idara za serikali.

“Kila abiria atakayebebwa na tuktuk lazima ajifunge mkanda wa usalama kila wakati. Pia, hataabiri tuktuk ambayo tayari imewabeba abiria waliopita idadi iliyoruhusiwa (watu watatu),” unaeleza mswada huo.

Kulingana na wadadisi, huenda masharti hayo mapya yakaathiri umaarufu wa Rais William Ruto miongoni mwa wahudumu wa bobaboda nchini, ikizingatiwa walikuwa miongoni mwa wale waliompigia kura kwa wingi kwenye uchaguzi wa Agosti 9 mwaka uliopita.

Kwenye kampeni zake, Rais Ruto na viongozi wa Kenya Kwanza walisema wangefanya kila wawezalo kuhakikisha wamebuni mazingira mwafaka ya kibiashara.

“Tutakuwa serikali ya kuwatetea mahasla (watu wa kiwango cha chini) kwa kuwaboreshea mazingira ya kuendesha biashara zao,” alisema Rais Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Hasla: Wachuuzi 40 wazuiwa kufanya biashara zao mjini

Mbunge Salasya aanikwa kwa kuruka deni

T L