• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:47 PM
Mbunge Salasya aanikwa kwa kuruka deni

Mbunge Salasya aanikwa kwa kuruka deni

Na LABAAN SHABAAN

Mbunge wa Mumias Mashariki Bw Peter Salasya ameanikwa paruwanja kwa madai ya kukwepa deni la Sh165,000 alipokuwa anafanya kazi na Banki ya Diamond Trust mwaka wa 2017.

Mmoja wa wadhamini watatu wa mkopo (Bw Polycarp Nyonje) aliyekerwa na mchezo wa paka na panya wa Bw Salasya amesema mbunge huyo amekuwa mtoro aliyeingia mitini baada ya kupokea mkopo.

“Nimefika Bunge la Kitaifa na afisi ya Ombudsman lakini sijapata msaada. Kila wakati tulipozungumza ana kwa ana na kupitia simu alizidi kuahidi atalipa deni hadi alipokuwa mbunge,” alisema Bw Nyonje alipomshtaki Bw Salasya kwa mwanaharakati wa haki za binadamu Bw Boniface Mwangi katika mtandao wa kijamii wa X.

Kwa mujibu wa waliodhulumiwa, kilio hiki cha haki kadhalika kilifikishwa hadi Chama cha Democratic Action (DAP) walipogundua mbunge huyo amedinda kupokea simu zao na kujibu arafa.

 “Akiba tuliyotolea jasho imekatwa kufikia kima cha Sh40, 821 na tukio hili limeathiri uwezo wetu wa kifedha katika Ushirika wa Akiba na Mikopo (sacco),” alilalamika Bw Nyonje hadi kilio kikavutia Mbunge Salasya aliyetoa mjibizo mtandaoni.

Katika akaunti yake ya X Bw Salasya amekejeli akikiri kuwepo kwa deni na akasema yuko tayari kulipa.

Ujumbe wa Salasya kupitia akaunti yake ya Twitter kuhusu malalamishi ya kukwepa deni. Picha|Labaan Shabaan

“Asante kwa kunitambisha Twitter na umwambie aje nimpe pesa zake Sh40,000,” Bw Salasya alimjibu Bw Mwangi.

“Mmenikumbusha nina deni na nimekuwa na kazi nyingi za eneobunge. Mwambie aje katika ofisi yangu Mumias Mashariki nilipe madeni yote nitakaporejea kutoka Nigeria,” aliongeza.

Kashfa hii imeonekana kumkera sana mbunge Salasya kwa sababu imemsukuma kupakia misururu ya jumbe mitandaoni pamoja na kurekodi video akimshambulia Bw Boniface kwa kuifichua pamoja na kurusha cheche zake dhidi ya wakenya walioghadhabishwa na habari hii.

  • Tags

You can share this post!

Bakora ya serikali sasa yaangukia bodaboda

Apu na teknolojia za kidijitali kuboresha kilimo na ufugaji

T L