• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
BBI: Wito viongozi wote wa Murang’a wazungumze kwa sauti moja

BBI: Wito viongozi wote wa Murang’a wazungumze kwa sauti moja

Na LAWRENCE ONGARO

VIONGOZI wa Murang’a na wadau wengine muhimu wa eneo hilo wamejumuika katika hoteli moja mjini Thika kujadili ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI).

Wakiongozwa na Gavana wa Murang’a, Mwangi Wa Iria viongozi hao walipitia ripoti hiyo ya BBI huku wakijiandaa kwa mkutano wa Rais mjini Sagana unaotarajiwa mnamo Jumamosi.

Bw Wa Iria amesema kila kiongozi alikuwa amealikwa katika mkutano huo na hakuna haja ya kulalamika eti hukualikwa.

“Sisi kama viongozi wa Murang’a tunamualika kila kiongozi kutoka eneo la Mlima Kenya ili tujadiliane ripoti ya BBI kwa msimamo moja,” alisema Bw Wa Iria.

Amesema mkutano wa leo Alhamisi ulikuwa wa kuwahamasisha viongozi wasome ripoti ya BBI kwa makini ili kuelewa yaliyomo.

“Vitabu vya BBI viko tayari na kwa hivyo kila kiongozi atapata nafasi ya kuipitia na kuielewa ili akienda mashinani mwananchi wa kawaida awe na nafasi ya kuielewa kwa makini,” amesema Bw Wa Iria.

Amesema baada ya mkutano wa leo Alhamisi viongozi sasa wana jukumu la kumfikia mwananchi na kumuelimisha kwa makini ripoti hiyo.

Baadhi ya washiriki wa mkutano wa Murang’a, Januari 28, 2021. Picha/ Lawrence Ongaro

Ametoa wito kwa jamii ya Mlima Kenya kufuata mwelekeo ambao Rais Uhuru Kenyatta atawaletea.

“Sisi kama jamii ya Mlima Kenya tunastahili kuwa kitu kimoja na kufuata mwelekeo mmoja tunaopewa na Rais,” amesema gavana huyo.

Amesema kwa wakati huu wanataka kuungana viongozi wote wa Murang’a wakiwemo wale waliopoteza nyadhifa zao.

“Tunataka kuweka kamati ya viongozi wachache ambao wataendeleza mwelekeo wa jinsi ya kumfikia mwananchi wa kawaida. Mpango huo utatupa mwelekeo utakaofanya mwananchi kuelewa ripoti ya BBI,” amesema Wa Iria.

Amesema wanataka kuhakikisha ya kwamba watakapokutana na Rais Kenyatta katika ikulu ndogo ya Sagana wawe wakizungumza kwa sauti moja bila mabishano yoyote.

Mbunge wa Kangema Bw Kigano Muturi amesema wataenda Sagana na sauti moja ya kuunga BBI.

Amewataka viongozi ‘wanaoeneza propaganda’ wasiendelee kupotosha wananchi.

“Sisi kama viongozi wa kutoka Mlima Kenya tunaelewa ripoti hiyo inanufaisha eneo letu pakubwa,” akasema Bw Muturi.

  • Tags

You can share this post!

Sagan Tosu anayochezea Mkenya Ismael Dunga yaanza...

BI TAIFA JANUARI 28, 2021