• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:50 AM
Benki ya Equity yafadhili wanafunzi 167 Kiambu

Benki ya Equity yafadhili wanafunzi 167 Kiambu

Na LAWRENCE ONGARO

WANAFUNZI wapatao 167 kutoka Kaunti ya Kiambu, wamenufaika na mpango wa Wings to Fly na Elimu Scholarship.

Wanafunzi hao wanaotarajia kujiunga na Kidato cha Kwanza, walijumuika wote katika Shule ya Upili ya Thika mnamo Ijumaa.

Mkurugenzi wa Benki ya Equity Bw Gerald Warui, alieleza kuwa wanafunzi walionufaika na mradi huo ni wale werevu na wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini.

Alizidi kueleza kuwa jumla ya majina 700 ya wanafunzi hao yaliwasilishwa kwa minajili ya kutaka ufadhili huo lakini iliwalazimu kuwachuja hadi kiwango fulani.

“Mradi huo unachukua jukumu la kuwasomesha wanafunzi hao kwa muda wa miaka minne huku wakilipiwa karo, wakipokea fedha za matumizi na hata za usafiri,” alifafanua mkurugenzi huyo.

Alieleza kuwa mradi huo unaangazia sana wanafunzi kutoka shule za umma na kote nchini wakiwa wamefadhili wanafunzi wapatao 19,000.

Aliwashauri wawe mstari wa mbele kusoma kwa bidii ili kuafikia malengo yao ya kuwa wanafunzi wa kutegemewa siku za usoni.

Wengi wa wanafunzi waliohojiwa walikiri ya kwamba wako tayari kuzamia kwenye masomo wakiwa na matumaini ya kufaulu katika malengo yao.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na naibu gavana wa Kiambu Bi Joyce Ngugi ambaye alipongeza Benki ya Equity kwa kuonyesha ukarimu wao wa kufadhili wanafunzi hao.

Aliwahimiza wanafunzi hao kujizatiti na kufanya bidii katika masomo yao.

“Nyinyi wanafunzi msikubali kupotoshwa na kuingilia mambo maovu kama utumizi wa dawa za kulevya,” alisema Bi Ngugi.

Alisema Kaunti ya Kiambu pia itafanya juhudi kuona ya kwamba inawasaidia wanafunzi ambao hawajafanikiwa kwa kupata ufadhili wa mradi wa Wings to Fly ama Elimu Scholarship programme.

Alisema kulingana na mpango huo, watafanya juhudi kuona ya kwamba kila mwanafunazi anapata haki yake ya ufadhili.

Mwanafunazi Anthony Muthoka aliyezoa alama 350 anasema amepata nafasi kujiunga na Shule ya Upili ya Ichagaki na anatarajia kufanya vyema masomoni.

You can share this post!

TAHARIRI: Bunge liharakishe sheria ya umasikini

Vyombo vya habari vyahimizwa visaidie NLC kuangazia masuala...