• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
Chiloba sasa ateuliwa kinara wa Mamlaka ya Mawasiliano

Chiloba sasa ateuliwa kinara wa Mamlaka ya Mawasiliano

Na SAMMY WAWERU

ALIYEKUWA Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Ezra Chiloba Jumane jioni aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Nchini(CA).

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari Jumanne, CA ilisema imemteua Bw Chiloba baada ya kufuzu kufuatia maombi ya waliomezea mate wadhifa huo iliotaja ulikuwa na ushindani mkuu.

Bw Chiloba na ambaye aliondolewa afisini na IEBC 2018 kwa madai kuwa alipatikana na makosa ya kukiuka mikakati ya utoaji zabuni katika uchaguzi mkuu wa 2017 na marudio ya urais, atahudumu kwa kipindi cha miaka minne.

Baada ya kukamilisha kipindi hicho, anaweza kuomba upya awamu nyingine kuhudumu.

“Bw Chiloba ni mshauri wa mikakati na mshirika wa kampuni ya Chil & Kemp, na vilevile wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya,” inasema taarifa iliyotumwa na mwenyekiti wa CA, Bw Kembi Gitura.

Chiloba amemrithi Bi Mercy Wanjau aliyehudumu kama Kaimu Mkurugenzi Mkuu, baada ya awamu ya Francis Wangusi kukamilika Agosti 2019.

Bw Chiloba ana Shahada ya Digrii kuhusu masuala ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN), Shahada ya Uzamili masuala ya sanaa kutoka Central European University, Hungary na Shahada nyingine ya Uzamili kuhusu Sayansi kutoka Chuo Kikuu cha Oxford.

Taarifa hiyo pia ilisema ana stashahada katika masuala ya blokcheni, teknolojia inayosifiwa mono duniani kwa uwezo wake wa kuzima wizi wa kura.

You can share this post!

Ripoti yaibua wasiwasi kuhusu utunzaji wa nguruwe

Yaibuka Mfanyabiashara wa Sudan kusini raia wa Kenya...