• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Ripoti yaibua wasiwasi kuhusu utunzaji wa nguruwe

Ripoti yaibua wasiwasi kuhusu utunzaji wa nguruwe

Na SAMMY WAWERU

UBORA wa nyama za nguruwe unategemea malezi, namna ya kuwasafirisha kuelekea kichinjioni na wanavyotunzwa kabla ya kuchinjwa.

Shirika la Kimataifa Kutetea haki za Mifugo na Wanyamapori, lisilo la kiserikali, linasema kuna uhusiano wa jinsi nguruwe wanafugwa, kuhudumiwa na nyama zake.

Kwenye ripoti ya hivi punde ya shirika hilo, World Animal Protection, ubora wa nyama za nguruwe unategemea wanavyotunzwa wakati wa ufugaji, kuwasifirisha buchari na wanavyohudumiwa kabla ya kuchinjwa.

Ripoti hiyo ilitolewa baada ya utafiti uliofanywa katika kichinjio cha Ndumbu-ini, kilichoko eneo la Kabete, Kiambu na kiungani mwa jiji la Nairobi, kuonyesha asilimia 25.83 ya nyama za nguruwe ni za ubora wa chini.

Buchari hiyo husambaza nyama zake katika mitaa mbalimbali Kaunti ya Nairobi. World Animal Protection ilishirikiana na Taasisi ya Kimataifa katika Utafiti wa Mifugo (ILRI) na Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN), kufanya utafiti huo na uliotekelezwa kati ya Januari 5 na Machi 2021.

Mfugaji wa nguruwe Kaunti ya Kiambu…PICHA/ SAMMY WAWERU

Yakizua hali ya wasiwasi kuhusu usafirishaji wa mifugo, matokeo yanafichua kwamba asilimia 27.7 ya nguruwe walisafirishwa kwa njia isiyofaa, wengi wakifungwa kwenye pikipiki hivyo basi kuhisi uchungu na kusababisha nyama kuwa duni.

Waliobebwa kwa kutumia magari, walisongamana.Utafiti huo pia unaonyesha asilimia 52 ya nguruwe waliwekwa zaidi ya saa 24 kichinjioni baada ya kununuliwa, ikizingatiwa walivyosafirishwa kuibua maswali.

Mifugo hawapaswi kuwekwa zaidi ya saa 18 kichinjioni, shirika hilo likisisitiza kwamba chini ya muda huo wanapasa kupewa chakula na maji ya kutosha.

Utafiti wa World Animal Protection pia unaonyesha asilimia 20 ya nguruwe waliohusishwa na kutoka kwa wafugaji tofauti waliwekwa pamoja, jambo lililochangia kupigana wakitafuta nafasi ya kutosha kujituliza, hivyo basi kusababisha majeraha.

“Maslahi ya mifugo yanapopuuzwa, kilele chake kitaishia kuwa na nyama za ubora wa chini. Haki za mifugo na wanyama zitiliwe maanani,” akasema Dkt Victor Yamo, Meneja wa Masuala ya Kampeni ya Mifugo katika shirika hilo, wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo kupitia hafla iliyoandaliwa kwa njia ya mtandao wa Zoom.

Matokeo ya utafiti huo yaliibua maswali wanyama wanavyopaswa kuchinjwa, Dkt Yamo akisema wanapochinjwa kwa njia isiyofaa huishia kuhisi uchungu kupita kiasi na kung’ang’ana.Kulingana na mtaalamu huyu, takriban asilimia 99 waliotumika katika utafiti walichinjwa vibaya.

“Wanyama wanapochinjwa kwa njia isiyofaa huzongwa na msongo wa mawazo na kuachilia homoni ya adrenaline na asidi ya lactic, chembechembe ambazo huharibu ubora wa nyama,” Dkt Yamo akasema, akihimiza wafugaji na wafanyabiashara kuzingatia matunzo bora ya mifugo na mifumo ya kuwasafirisha kuelekea vichinjioni.

“Nyama za mifugo waliozongwa na msongo wa mawazo hazina maji ya kutosha, hivyo basi kuwa mbovu. Ni hasara kwa mfugaji na mfanyabiashara,” akaelezea daktari huyo wa mifugo.

Alisema uchunguzi wao unaonyesha nguruwe wengi huwekwa alama kwa kukatwa na kifaa chenye makali wakati wakisubiri kuchinjwa, ili kuwatambua.

Hatimaye, tendo hilo huwasababishia uchungu usiomithilika na nguruwe kuogopa.

Alisema alama hizo ni mwanya wa uchafu na bakteria kuingia, hivyo basi kuchangia nyama kuwa hatari.

 

  • Tags

You can share this post!

Mkulima anavyokabili kero ya mazao mbichi ya shambani...

Chiloba sasa ateuliwa kinara wa Mamlaka ya Mawasiliano