• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:55 AM
Chini ya asilimia 10 ya mazao ya shambani yanayouzwa nje ya nchi yanaongezwa thamani – tafiti za shirika

Chini ya asilimia 10 ya mazao ya shambani yanayouzwa nje ya nchi yanaongezwa thamani – tafiti za shirika

Na SAMMY WAWERU

WAKULIMA Kenya wamehimizwa kukumbatia mfumo wa uongezaji mazao thamani kwa sababu yaliyosindikwa yana mapato mazuri ndani na nje ya nchi.

Shirika moja la kutafutia wakulima soko, ndilo Fairtrade Africa (FTA) limesema bidhaa zilizoongezwa thamani zina soko lenye ushindani mkubwa.

FTA ni muungano unaojumuisha mashirika na vyama vya ushirika vilivyosajiliwa kuendeleza shughuli za kilimo, pamoja na wakulima Barani Afrika na pia nje ya bara ambapo huwatafutia soko katika mataifa ya ughaibuni.

Shirika hilo kwa sasa lina nchi 33 wanachama, ambapo huunganisha wakulima na masoko yenye ushindani mkuu.Nchi zinazofaidika kupitia FTA ni pamoja na Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Ethiopia, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Burundi.

“Mazao yaliyoungezwa thamani, mapato yanakuwa hadi mara tatu,”akasema Bi Kate Nkatha, Mkurugenzi Mkuu wa Mauzo FTA katika hafla iliyoandaliwa jijini Nairobi na iliyoleta pamoja wakulima na wazalishaji.

Mkurugenzi Mkuu wa Mauzo Freetrade Africa (FTA), Bi Kate Nkatha akihutubu katika hafla jijini Nairobi iliyoleta pamoja wakulima na mashirika yanayoendeleza kilimo…PICHA/ SAMMY WAWERU

Aidha, shirika hilo lina zaidi ya wakulima milioni 1.8 kote ulimwenguni, 450, 000 wakitoka Kenya.Bi Nkatha alisema lina soko tayari Ujerumani, Uholanzi, Canada, Finland, Ufaransa, Ubelgiji, Luxembourg, Italia, Australia, Norway, Sweden, Switzerland na Uingereza, kati ya mataifa mengine.

Kwa sasa, FTA inasaka mianya kuingia Korea, China na Japan.“Mazao tunayotafutia soko hupitia kwa wafanyabiashara rejareja, kisha yanafikia mlaji,” Bi Kate akaelezea, akisema hatua hiyo imesaidia kuondoa mtandao wa mawakala.

“Chini ya asilimia 10 ya mazao tunayouza ndiyo huongezwa thamani,” akasema, akihimiza wakulima kukumbatia mfumo wa uongezaji mazao thamani ili kunogesha soko.Kenya huuza majanichai, kahawa na maua kwa wingi katika masoko ya kigeni.

“Hata hivyo, tumeona mazao mabichi ya shambani yasiyochukua muda mrefu kuzalisha, mazao ya kuku na ng’ombe na pia bidhaa zilizoongezwa thamani, yana mianya bora ya soko,” afisa huyo akasema.

  • Tags

You can share this post!

Meru kuendelea kufaidi mradi wa kuboresha kilimo cha viazi

Mradi wa maji wakatizwa na matapeli mtaani Mukuru na...