• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Dalili zajitokeza huenda Karua yupo kwenye kibaridi Azimio

Dalili zajitokeza huenda Karua yupo kwenye kibaridi Azimio

NA WANDERI KAMAU

DALILI zimeanza kujitokeza kuwa huenda kiongozi wa Narc-Kenya, Bi Martha Karua hafahamu vyema hatima yake ya kisiasa ndani ya mrengo wa Azimio la Umoja, licha ya kuwa miongoni mwa vigogo wakuu katika muungano huo.

Katika siku za hivi karibuni, Bi Karua hajawa akionekana kushirikishwa kwenye shughuli muhimu za kisiasa za Azimio, licha ya kuhudumu kama mgombea-mwenza wa kiongozi wa mrengo huo, Bw Raila Odinga, kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9, mwaka uliopita.

Kulingana na wadadisi, ishara ya kwanza iliyoonyesha Bi Karua “ameanza kutengwa kisiasa” katika mrengo huo, ni hatua yake ya kutojumuishwa kwenye kamati ya Azimio inayoshiriki kwenye Mazungumzo ya Maridhiano yanayoendelea katika Ukumbi wa Bomas, Nairobi.

Japo awali ilitarajiwa kuwa Bw Odinga angemteua Bi Karua kuongoza ujumbe wa Azimio katika mazungumzo hayo, aliwashangaza wengi baada ya kumteuakkiongozi wa chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, kuwa kiongozi wa ujumbe huo.

Mbali na Bw Musyoka, viongozi wengine wanaowakilisha Azimio kwenye mazungumzo hayo ni Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa, mbunge Amina Mnyazi (Malindi) na Seneta Okong’o Omogeni (Nyamira).

Baada ya malalamishi kuibuka kuwa Bw Odinga amelitenga eneo la Mlima Kenya kwa kutomteua mtu yeyote kutoka eneo hilo katika ujumbe huo, aliteua kikosi cha kiufundi, ikitarajiwa angemteua Bi Karua.

Hata hivyo, alimteua Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Jeremiah Kioni, kuongoza kikosi hicho, kinachowashirikisha watu wannne.

Mbali na Bw Kioni, wanachama wengine wa kikosi hicho ni Dkt Adams Oloo, Bw Zein Abubakar na Bi Isabel Githinji.

Wadadisi wanasema hilo ndilo lililoashiria kuwa Bw Odinga ameonyesha dalili za kutoridhika na mchango wa kisiasa aliotoa Bi Karua katika mrengo huo.

“Hilo ndilo lilianza kuashiria kuwa kuna hali ya mvutano katika Azimio kwani kimsingi, Bi Karua anashikilia nafasi kubwa katika mrengo huo kama kigogo-mwenza, kuliko Bw Kioni. Ikiwa Bw Raila angezingatia utaratibu wa kiitifaki, nafasi hiyo ingechukuliwa na Bi Karua,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Ishara ya mvutano baina ya Bw Musyoka na Bi Karua ilijitokeza Jumapili baada ya Bi Karua kupinga ripoti za magazetini zilizomnukuu Bw Musyoka kwamba “Azimio sasa inamtambua Dkt William Ruto kama Rais wa Kenya”.

Akanukuliwa Bw Musyoka: “Tunamshukuru Rais kwa kushusha msimamo wake na kuunga mkono mazungumzo ya maridhiano. Kutokana na msimamo wake (Ruto), tunamtambua huku tukiendelea kusubiri mustakabali mwema, kwani nani ajuaye kuhusu ikiwa Mungu atakuwa nasi?”

Aliripotiwa kutoa kauli hiyo Jumamosi, alipohutubu katika eneo la Voi, Kaunti ya Taita Taveta.
Hata hivyo, Jumapili, Bi Karua alipinga kauli hiyo, akiitaja kutokuwa msimamo wa Azimio.
“Si kweli,” akasema Bi Karua kupitia mtandao wa X (zamani kama Twitter).

Baadaye, Bw Musyoka alitoa taarifa akisema kuwa “alinukuliwa visivyo”.

“Nimebaini kuwa baadhi ya vyombo vya habari vimeninukuu isivyofaa kuhusu hali ya nchi, hasa uhalali wa utawala huu. Kama Azimio, msimamo wetu ni kuwa lazima uchaguzi wa urais wa mwaka uliopita uchunguzwe kwa kina,” akasema Bw Musyoka, akionekana kutokanusha kauli yake.

Kulingana na wadadisi, sababu nyingine ambayo imemfanya Bw Odinga kuonekana kumtenga kisiasa Bi Karua ni kuongezeka kwa umaarufu na ushawishi wa kisiasa wa Naibu Rais Rigathi Gachagua katika eneo la Mlima Kenya.

Wanasema mwelekeo huo ndio, pamoja na idadi chache ya kura alizopata kutoka eneo hilo kwenye uchaguzi wa 2022, ndizo zimemfanya Bw Odinga kutomtegemea pakubwa Bi Karua kuendeleza ajenda yake ya kisiasa.

“Bila shaka, ni wazi kuwa Bw Gachagua amejijenga sana kisiasa Mlima Kenya. Kimsingi, amejizolea ufuasi mkubwa miongoni mwa wakazi, ikizingatiwa anatumia ushawishi wa kuwa serikalini. Katika hali hii, ni wazi kuwa ni watu wachache watamuunga mkono Bi Karua, kwa kuhofia kuachwa kwenye baridi ya kisiasa. Hivyo, Bw Odinga anaogopa kukabiliana na wimbi la kisiasa la Bw Gachagua,” akasema Bw Mutai.

Juhudi zetu za kuwasiliana na Bi Karua hapo jana hazikufua dafu, kwani hakujibu jumbe wala kuchukua simu zetu.

  • Tags

You can share this post!

Wetang’ula atetea kusafirisha wafisadi mbinguni

Tanzia: Shujaa wa Maumau Muthoni wa Kirima aaga dunia

T L