• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Wetang’ula atetea kusafirisha wafisadi mbinguni

Wetang’ula atetea kusafirisha wafisadi mbinguni

CHARLES WASONGA na DICKSON MWITI

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula ametetea mbinu kali ambazo Rais William Ruto ametangaza kuzitumia kupambana na wafisadi nchini.

Bw Wetang’ula alisema mbinu za kuwafurusha, kuwasukuma gerezani au kusafirisha mbinguni washiriki uovu huo ni halisi na zimewahi kutumika katika nchi zingine kuonyesha kujitolea kumaliza ufisadi.

Alisema katika nchi ya Japan, kwa mfano, mtu anayetenda uhalifu unaowaathiri watu wengi, hufanya kitendo kinachojulikana kama, “harakiri”, ambacho ni sasa na kujiua.

“Hii ni sawa na kujipeleka mbinguni ikiwa umewakosea watu,” Bw Wetang’ula akasema.

“Wale ambao sio waraibu wa kusoma vitabu, kama baadhi yetu, wanaweza kufasiri kauli ya Rais kuwa ataua watu. Rais hana historia ya kuua watu na hatarajii kuanza kufanya kitu ambacho hajawahi kukifanya,” akaeleza.

Spika Wetang’ula alitoa kauli hiyo Jumapili Septemba 3, 2023 alipoongoza hafla ya kuchanga fedha katika Shule ya Upili ya KK Tharaine, iliyoko eneo bunge la Tigania Magharibi, Kaunti ya Meru.

Wiki jana, Rais Ruto alitoa onyo kali kwa wafisadi, haswa wale walioporomosha kampuni ya sukari Mumias, akisema atapambana nao kwa njia tatu; kuwafurusha kutoka Kenya, kuwasukuma gerezani au kuwasafirisha mbinguni.

Alitoa onyo hilo wakati wa ziara yake ya siku tano eneo la Magharibi mwa Kenya.

Viongozi wa upinzani, wakiongozwa na kinara wao, Raila Odinga, wamemkashifu kiongozi wa kitaifa wakisema mbinu hiyo ni dhalimu na inakiuka Katiba na sheria husika.

Lakini akiendelea kumtetea Dkt Ruto, Bw Wetang’ula, alirejelea historia ya Roma, akisema kiongozi huyo anao wajibu wa kulinda yale ambayo ni mazuri kwa umma na “atakuwa amefeli kama kiongozi asipofanya hivyo.”

“Hii ndio ambacho Rais alikuwa akirejelea aliposema wafisadi sharti waende gerezani, kwa maana kwamba watapitishwa kortini. Unaondoka nje ya nchi ikiwa wewe sio Mkenya au unajipeleka mbinguni kwa njia zake,” akasema Wetang’ula.

Akaongeza: “Lakini jambo muhimu sio kujikita katika semi zenye mafumbo, lakini ujumbe ambao Rais alikuwa akiupitisha. Wenye masikio walisikie lakini pia tumeona wanaoupinga.”

Bw Wetang’ula alisisitiza kuwa mtu yeyote anayetetea ufisadi ni adui wa Kenya kwani ajenda ya serikali ni kuhakikisha kuwa pesa za walipa ushuru zinatumika katika miradi muhimu ya maendeleo inavyotakikana.

Aliongeza kuwa Rais amekuwa akifanya ziara kote nchini akihubiri amani na kukagua miradi ya maendeleo.

Alisema hivyo ndivyo inapasa akikariri kwamba inaonyesha kuwa Dkt Ruto anajali kuhusu yale yanayofanyika katika pembe zote za taifa hili.

“Tunapaswa kudumisha amani ili kujenga taifa letu na tupambane na ufisadi kila mahali na popote tunapoushuhudia,” Bw Wetang’ula akasema.

Spika huyo aliandamana na wabunge;  Martin Wanyonyi (Webuye Mashariki), George Kariuki (Ndia), Njoki Njeru (Mbunge Mwakilishi wa Embu), Kirima Nguchine (Imenti ya Kati), Mugambi Rindikiiri (Buuri), Mpuru Aburi (Tigania Mashariki), Dan Kiili (Igembe Central), Julius Taitumu (Igembe Kaskazini), Dorothy Muthoni (Mbunge Maalum) na mwenyeji wake, John Mutunga.

  • Tags

You can share this post!

Biashara ya nyama inachangia mazingira kuzorota, kongamano...

Dalili zajitokeza huenda Karua yupo kwenye kibaridi Azimio

T L