• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:32 PM
Daraja jipya latarajiwa kuinua uchumi wa Kilifi

Daraja jipya latarajiwa kuinua uchumi wa Kilifi

Na MAUREEN ONGALA

WAKAZI wa maeneo ya Baricho na Lango Baya katika Kaunti ya Kilifi wameelezea matumaini kwamba mradi unaoendelea wa ujenzi wa daraja la kuvukia mto Galana utachochea ukuaji wa kiuchumi katika maeneo hayo.

Mradi huo kwa jina, Baricho Bridge Project, ulianza 2018 na unatarajiwa kugharimu Sh2.3 bilioni utakapokamilishwa.

Daraja hilo ni la urefu wa mita 241.

Kwa miongo kadha wakazi wamekuwa wakihatarisha maisha yao wakivuka mto huo, wenye mamba na viboko hatari, wakiendelea na shughuli za kujitafutia riziki.

Hali huwa mbaya zaidi katika msimu wa mvua nyingi mto huo unapofurika na hivyo wakazi kulazimika kutumia mashua kuvuka mto huo.Kuna nyakati ambapo mashua husombwa na maji ya mto huo.

Ujenzi wa barabara hiyo unaendeshwa na kampuni ya MS China No 10 Enginering Group na utaunganisha kaunti ndogo za Magarini na Malindi utakapokamilika mnamo Aprili 2022.

Bw Manyeso Kamcha alisema maafa mengi yameshuhudiwa katika eneo hilo baada ya wakazi kushambuliwa na wanyamapori.

Alisema tangu mkandarasi huyo alipoanza kutengeneza daraja hilo, visa vya watu kuvuka mto huo kwa miguu au mashua vimepungua.

Bw Kamcha alisema wakazi wengi hutumia daraja la muda kuvuka mto huo chini ya uangalizi wa mwanakandarasi huyo ili kuzuia mikasa.

“Huwa tunalipa Sh200 na Sh400 kwa mashua kuvuka kati ya Baricho na Lango Baya. Wakazi wengi hawawezi kumudu kulipa nauli hiyo na hivyo huamua kuvuka kwa miguu na hivyo kuhatarisha maisha yao,” akasema.

Kulingana na Kamcha, wakulima na wafanyabiashara wataweza kusafirisha bidhaa zao bila changamoto ilivyokuwa zamani, ujenzi wa daraja hilo utakapokamilika.

Wakulima katika maeneo hayo hukuza mboga na matunda ambayo wao huuza katika masoko ya miji ya Malindi na Kilifi.

“Tutafanya biashara kwa urahisi. Tutaimarisha mapato yetu na kupunguza umasikini,” Bw Kamcha akasema.

Aliongeza kuwa idadi ya viboko na mamba huongezeka mto Galana unapofurika hali inayochangia ongezeko la watu kushambuliwa na kuuawa na wanyama hao.

Bw Kamcha aliitaka serikali kuu na mkandarasi kuharakisha ujenzi wa daraja hilo ili kuokoa maisha ya wakazi.

“Mwafaa kukamilisha ujenzi wa daraja hili ili tuweze kulitumia ili tusishambuliwa na wanyama hawa wa majini,” akaeleza.

Bw Jumwa Charo alisema watoto wadogo ndio huathirika zaidi wanapovuka mto huo.

“Tumeshuhudia visa vingi ambapo watoto husombwa na maji ya mto huku wengine wakishambuliwa na mamba na viboko. Wengine wanaishi na majeraha baada ya kushambuliwa na wanyama hawa,” akasema.

You can share this post!

Kenya yapokonya wavuvi wa China leseni kwa kutesa Wakenya

Munya atetea KTDA kuhusu bonasi ya chini ya majani chai