• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Munya atetea KTDA kuhusu bonasi ya chini ya majani chai

Munya atetea KTDA kuhusu bonasi ya chini ya majani chai

Na IRENE MUGO

WAZIRI Kilimo Peter Munya ametetea Mamlaka ya Kilimo cha Majanichai (KTDA) kuhusu malipo ya chini ya bonasi kwa wakulima mwaka huu 2021, akisema Hazina ya Kusawazisha bei ya zao hilo itaboresha malipo hayo mwaka 2022.

Hazina hiyo itawapa wakulipa pesa za kununua pembejeo za kilimo na kuhakikisha kuwa mapato yao hayashuki hata kama bei ya majanichai ni duni katika masoko ya kimataifa.

Bw Munya alisema kuwa bonasi ya chini kwa wakulima mwaka huu ilitokana na bei duni ya majanichai katika mnada wa Mombasa ambayo ilikuwa imewekwa na mawakala wenye nia ya kuwafilisi wakulima jasho lao.

“Wakulima hawafai kulalamika kuhusu bonasi ya chini kwa sababu hali hiyo ilichangiwa na mawakala wakora wakishirikiana na baadhi ya wakurugenzi wa KTDA. Hata hivyo, hili ni suala ambalo limetatuliwa na mwaka ujao, wakulima hawatalipwa bonasi ya chini tena,” akasema Bw Munya aliyekuwa akizungumza mjini Nyeri baada ya kuzuru kiwanda cha majanichai cha Iria-Ini.

“Serikali imesawazisha bei ya majanichai kuwaokoa na kuwalinda wakulima. Mtindo ambao tumeukumbatia wa kuweka bei hiyo kwa wanunuzi unafaa na utasaidia kuhakikisha haipungui hata kama kuna mabadiliko katika bei ya nje,” akaongeza Bw Munya.

Wakati huo huo, Bw Munya alisema wakulima wamekuwa wakilemewa na umaskini kutokana na mikopo inayotoza riba ya juu ambayo wamekuwa wakipewa na kampuni ya Green Fedha, mshirika wa KTDA.

“Kufikia Disemba mkopo wowote ambao unatolewa kwa mkulipa hautakuwa ukitoza riba zaidi ya asilimia 21. Tumepunguza kiwango hicho hadi asilimia nane na baada ya bei iliyosawazishwa kuanza kutekelezwa, itashuka hadi asilimia tano,” akasema Bw Munya.

Vilevile, waziri huyo alisema serikali inapanga kuanzisha maabara ambayo itakuwa ikipima ubora wa majanichai ya Kenya kabla ya kuuzwa katika masoko ya nje.

“Kwa sasa ni majanichai pekee ambayo inauzwa bila ubora wake kupimwa tofauti na kahawa na mazao mengine. Baada ya maabara hayo kujengwa, tutathmini ubora wa majanichai ambao utakikisha wakulima wanalipwa bonasi za juu,”alisema.

You can share this post!

Daraja jipya latarajiwa kuinua uchumi wa Kilifi

Muhsin aombolezwa kama shujaa wa uanahabari, kukuza...