• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:05 PM
Kenya yapokonya wavuvi wa China leseni kwa kutesa Wakenya

Kenya yapokonya wavuvi wa China leseni kwa kutesa Wakenya

Na ANTHONY KITIMO

KENYA imefutilia mbali leseni za meli sita za uvuvi za China kwa madai kwamba zilikuwa zikidhulumu mabaharia wa Kenya na kutumia vifaa vya uvuvi vilivyopigwa marufuku.

Meli hizo zimekuwa zikiendeleza uvuvi baada ya kupata kibali kuendesha shughuli hiyo kuanzia Januari 1, 2021 hadi Desemba 31 2031.

Mkuu wa uvuvi katika Mamlaka ya shughuli za baharini ya Kenya (KMA), John Omingo alisema walipokonya meli hizo leseni kufuatia malalamishi kutoka kwa wafanyakazi Wakenya kwamba zinapuuza kanuni kadhaa za uvuvi za Kenya.

“KMA imeondoa leseni baada ya mapendekezo kutoka kwa mashirika tofauti kwa kukiuka sheria za uvuvi za Kenya. Meli hizo ni pamoja na LU Qing Yuan Yu 160, LU Qing Yuan Yu 158, LU Qing Yuan Yu 155, LU Qing Yuan Yu 157, LU Qing Yuan Yu 156 na LU Qing Yuan Yu 159,” alisema Bw Omingo.

Aliongeza: “Tayari tumewasiliana na wamiliki wa meli hizo ambao ni kampuni ya Qinsdad Yung Tung-Pelagic Fisheries Limited kuhusu kuondolewa kwa leseni zao.”

Baadhi ya wafanyakazi Wakenya walikiri kwamba wamekuwa wakitishiwa kutupwa kwenye bahari na wavuvi hao.

Kuondolewa kwa leseni hizo kunajiri wakati ambao Kenya inang’ang’ana kufuatilia shughuli katika bahari baada ya shirika la Ufaransa Collecte Localisation Satellites(CLS) kusimamisha huduma zake Kenya kwa kutolipwa zaidi ya Sh16 milioni.

You can share this post!

Matumaini tele kiwanda cha sukari kianze kunguruma tena

Daraja jipya latarajiwa kuinua uchumi wa Kilifi