• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:55 AM
Dhihirisheni ujuzi kupanda vyeo, wanawake waambiwa

Dhihirisheni ujuzi kupanda vyeo, wanawake waambiwa

NA LAWRENCE ONGARO

WANAWAKE wamehimizwa kuwa mstari wa mbele kujaza nafasi za uongozi hasa katika kampuni kubwakubwa.

Wametajwa kama kiungo cha kueneza maelewano na kuendeleza uongozi kwa njia inayostahili.

Hafla ya kusherehekea uongozi wa wanawake ilifanyika katika kampuni ya Delmonte majuzi huku wakipongezwa jinsi ambavyo wamebobea pakubwa katika nyanja za uongozi.

Meneja wa masoko katika Benki ya ABSA Bi Caroline Kendi alisema wanawake wana nafasi kubwa ya kujiendeleza katika maswala ya uongozi.

“Wanawake wasikubali kudunishwa katika maswala ya uongozi na kwa hivyo ninawashajiisha wenzangu wajitokeze kuonyesha ujuzi wao,” alifafanua Bi Kendi.

Alitetea wanawake kwa kusema kuwa wana umuhimu mkubwa katika jamii na ni shartu wawe mstari wa mbele na kutoa maoni yao ili watambulike.

Alitoa changamoto kwa wanawake kujitambulisha ili kuonekana katika nafasi za juu za uongozi.

Alisema kujitambulisha ni kuonyesha ujuzi wako ili ibainike wazi wewe ni bora.

Ilidaiwa ya kwamba wanawake wametajwa kama waamuzi wema kwa maswala muhimu za kikazi na kwa hivyo kila mara wapewe nafasi ya kuongoza.

Meneja wa ubora wa bidhaa Bi Hannah Kithuki alisema wanawake ni watu wa kuleta amani na ni muhimu kupewa nafasi ya kuonyesha ujuzi wao.

Alisema wakati kama huu tunaposhuhudia matatizo mengi nchini wanawake wana nafasi njema ya kujumuishwa katika maswala ya kuamua matatizo ya kijamii.

Meneja huyo alipendekeza wanawake waorodheshwe katika maswala ya maamuzi muhimu na wasikilizwe kwa makini.

Bi Sarah Ogongo naibu mkurugenzi wa uhusiano mwema katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) alisema wanawake ni watu wa kuaminika hasa katika familia ambapo wakati wa matatizo ya kijamii wao Ndio hushughulika na watoto na maswala ya kifamilia.

Alisema hata wakati wa misukosuko katika nataifa tofauti, wanawake Ndio huwa mstari wa mbele kulea watoto na kulinda familia.

Baadhi ya wanawake na wadau wengine wa kutetea wanawake wakiwa kwenye hafla iliyoandaliwa katika kampuni ya Delmonte, Thika. Wanawake wamehimizwa kuwa mstari wa mbele kujaza nafasi za uongozi hasa katika kampuni kubwakubwa. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Afisa wa uhusiano mwema katika kampuni ya Delmonte Kenya Ltd Bi Jackline Muthoni, alisema wanawake wanastahili kuketi katika nafasi za juu ili kutoa maamuzi muhimu.

“Wanawake wengi wamesoma hadi kiwango cha juu na kwa hivyo wana nafasi ya kuleta amani na kutumia busara wanapofanya maamuzi yao,” alisema Bi Muthoni.

Alisema wanawake hawafai kubaguliwa kwani maamuzi yao pia ni muhimu katika maswala ya kijamii.

“Kwa hivyo ni lazima tujadili kuhusu jinsi tutakavyowapa wanawake nafasi ya kujitetea bila kubaguliwa kijinsia,” alieleza afisa huyo.

  • Tags

You can share this post!

Jumba la wajawazito kujifungua lajengwa Gatundu Kaskazini

Masharti mapya ya maridhiano yazuka

T L