• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:02 PM
DPP kuunganisha kesi ya  mabwawa ya Kimwarer na Aror

DPP kuunganisha kesi ya mabwawa ya Kimwarer na Aror

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa mashtaka ya umma (DPP) Noordin Haji jana aliwasilisha ombi ya kuunganishwa kwa kesi ya ufisadi wa Sh63bilioni inayowakabili Waziri wa Fedha Henry Rotich na mkurugenzi mkuu wa zamani Shirika la Ustawi wa Kerio Valley (KVDA) David Kimosop.

Kesi hizi mbili zinatokana na kufujwa kwa pesa katika ujenzi wa mabwawa ya Kimwarer na Arror. Katika ombi hilo DPP amepunguza idadi ya washtakiwa kutoka 18 hadi tisa (9). Pia amepunguza mashtaka kutoka 40 hadi 30.

Akiwasilisha ombi hilo kiongozi maalum wa mashtaka Bw Taiba Ali Taib na naibu wa DPP Bw Alexander Muteti alimweleza hakimu mkuu mahakama Bw Lawrence Mugambi idadi ya mashahidi imepunguzwa kutoka 104 hadi 52.

“Lengo la kuwasilisha ombi hili la kuunganishwa kwa kesi hizi mbili  dhidi ya Bw Rotich na Bw Kimosop ni kuhakikisha imekamilishwa kwa haraka,”alisema Bw Muteti. Hakimu alifahamishwa mashahidi watakaofika katika kesi ya Bw Rotich na Bw Kimosop niwamoja tu.

Pia  afisi ya DPP imeeleza kuwa kesi hiyo itasikizwa kwa upesi. “DPP ameruhusiwa kisheria kuunganisha  kesi hizi mbili kupunguza muda ambao mahakama itachukua kuzisikiza,” alisema Bw Muteti.

Viongozi wa mashtaka Taib Ali Taib (kushoto) na Alexander Muteti…Picha/ RICHARD MUNGUTI

Kiiongozi huyo wa mashtaka alieleza mahakama kwamba rasilmali zitakazotumika zitapunguka kama vile kusafirisha mashahidi. Kwa sasa kuna kesi tatu kuhusu sakata hii ya mabwawa.

Bw Taib alieleza mahakama mnamo Mei mwaka huu afisi ya DPP ilitenganisha kesi hizi kuwa tatu ili zisikizwe na kuamuliwa kwa haraka. Miongoni mwa kesi hizi tatu ni pamoja na ile inayowakabili raia 18 wa Italia wanaomiliki kampuni ya CMC di Ravenna.

Raia hao 18 walikataa kufika nchini kujibu mashtaka dhidi yao. Mahakama ilitoa kibali cha kuwatia nguvuni Waitaliano hao. Maafisa wa polisi wa Kenya watashirikiana na wale wa kimataifa kuwakamata washtakiwa hao kutoka Italy.

Katika mashtaka hayo mapya 30 Bw Rotich ameshtakiwa pamoja na Mabw Kennedy Nyakundi Nyachiro,Jackson Njau Kinyanjui, David Kipchumba Kimosop,William KiPkemboi Maina, Paul Kipkoech Serem, Francis Chepkonga Kipkech, Titus Muriithi na Geoffrey Mwangi Wahungu.

Shtaka la kwanza dhidi ya tisa hao ni kwamba walikula njama kuifuja serikali Dola za Marekani 501,829,769 kwa kuidhinisha ujenzi wa mabwawa ya Kimwerer na Arror kinyume cha sheria. Lakini mawakili Kioko Kilukumi na Katwa Kigen walieleza hakimu watapinga hatua hiyo ya kuunganishwa kwa kesi hizo mbili dhidi ya Mabw Rotich na Kimosop.

Waliposhtakiwa washtakiwa hao walikanusha kesi dhidi yao na kuachiliwa kwa dhamana.

Mawakili Kilukumi na Kigen walieleza mahakama kesi hiyo lengo la kuwasilisha mashtaka hayo mapya ni kuchelewesha  kusikizwa kwa kesi hiyo. Bw Mugambi alielezwa tangu kesi hiyo iwasilishwe mahakamani imefanyiwa marekebisho mara tano.

Bw Muteti alijibu madai hayo akisema kumekuwa na kampeini mbaya dhidi ya DPP kuhusu utenda kazi na uendelezaji wa kesi. Bw Mugambi alihoji sababu ya kiongozi mmoja wa mashtaka kutoka mahakamani kabla ya maagizo ya kuunganishwa kwa kesi hizo kutolewa.

Bw Mugambi alimshutumu kiongozi huyo wa mashtaka akisema kesi hiyo iliitwa lakini hakukuwa na wakili wa serikali. Bw Muteti aliomba msahama na kusema kuna viongozi wa mashtaka wanane ambao wanaohusika na kesi.

Aliahidi makosa hayo hayatarudiwa tena. Bw Mugambi aliwaamuru wote wanaohusika waandae tetezi zao kabla Oktoba 25. Kesi hiyo itatajwa Oktoba 26 kwa njia ya mtandao ili hakimu atoe mwelekeo jinsi ombi hilo la DPP la kuunganishwa kesi hiyo itasikizwa.

Wakili Kioko Kilukumi (kushoto) anayemwakilisha Roticha…Picha/ RICHARD MUNGUTI

 

  • Tags

You can share this post!

Aussmes ataka kusajili walio na ujuzi

Haaland arejea kwa matao ya juu na kufungia Dortmund mabao...

T L