• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:50 AM
Haaland arejea kwa matao ya juu na kufungia Dortmund mabao mawili ligini

Haaland arejea kwa matao ya juu na kufungia Dortmund mabao mawili ligini

Na MASHIRIKA

ERLING Braut Haaland alifungia Borussia Dortmund mabao mawili katika mchuano uliokuwa wake wa kwanza kutandaza tangu apate jeraha la misuli ya mguu lililomweka mkekani kuanzia Septemba.

Mchango huo wa Haaland ulisaidia waajiri wake Dortmund kusajili ushindi wa 3-1 dhidi ya Mainz na kutua katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

Marco Reus aliwaweka Dortmund kifua mbele katika dakika ya tatu kabla ya Haaland kufunga penalti katika dakika ya 54 kisha kupachika wavuni goli lake la pili sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa.

Jonathan Burkardt alifutia Mainz machozi katika dakika ya 87. Kikosi hicho kwa sasa kinashikilia nafasi ya 11 jedwalini kwa alama 10.

Kufikia sasa, Haaland, 21, amefungia Dortmund mabao 49 kutokana na mechi 49 za Bundesliga. Ina maana kwamba nyota huyo wa zamani wa RB Salzburg nchini Austria kwa sasa amefungia Dortmund magoli 70 kutokana na michuano 68 ya mashindano yote.

“Ni wazi kwamba ndiye kiungo muhimu kilichokosekana katika timu yetu. Ni vyema achezeshwe katika takriban kila mechi kwa sababu wachezaji wawili au watatu wa kikosi pinzani ndio hulazimika kumkabili kila mara anapokuwa na mpira. Tukio hilo hutupa nafasi nyingi za wazi kufunga mabao kupitia kwa wanasoka wengine,” akasema Reus ambaye ni nahodha wa Dortmund.

Ushindi wa Dortmund ulikuwa wao wa tisa mfululizo kusajili ligini katika uwanja wao wa nyumbani wa Signal Iduna Park.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

DPP kuunganisha kesi ya mabwawa ya Kimwarer na Aror

NMG yatoa msaada wa vitabu kwa wanafunzi shuleni Kawangware

T L