• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Duale aitaka serikali ya Korane iimarishe huduma Garissa

Duale aitaka serikali ya Korane iimarishe huduma Garissa

Na FARHIYA HUSSEIN

MBUNGE wa Garissa Mjini, Aden Duale ameilaumu serikali ya Kaunti ya Garissa ikiongozwa na Gavana Ali Korane akisema huduma zinazidi kudorora.

Mbunge huyo ambaye alikuwa mstari wa mbele kumuunga mkono Bw Korane wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017 sasa amebadilisha maoni yake.

“Nilikuwa nikimuunga mkono Gavana Korane uchaguzi uliopita, kwa sababu nlimuamini ana uwezo wa kusaidia watu wa eneo hili. Lakini hiyo haifanyiki, huduma kwa wakazi wa huku zimezidi kuzorota,” Bw Duale, alisema katika mahojiano na stesheni moja eneo hilo.

Mbunge huyo alitaja sekta ya afya na maji kuwa miongoni za huduma zilizoathirika zaidi.

“Zaidi ya watu 21 wakiwemo wafanyikazi wa afya wamekufa kutokana na kirusi cha Korona sababu kuu ikiwa ukosefu wa oksijeni katika hospitali. Kulikuwa na maji katika kila sekta ya mji wa Garissa, leo mabomba ni kavu, ”alisema mbunge huyo.

Wakati huo huo, Bw Duale alimsifu Gavana wa zamani wa Garissa Nathif Jama kwa suala la utoaji wa huduma.

“Bw Jama alifanya kazi kubwa, aliboresha miundombinu ya huduma za afya. Dawa za matibabu zilipatikana katika sekta za vijijini. Lakini leo akina mama katika kitengo chetu cha ugatuzi wanabeba vifaa vyao wenyewe kutoka nyumbani wanapokwenda kwenye wodi za akina mama, ” Bw Duale akasema.

Mbunge huyo aliweka wazi kuwa hatowania utawala wa serikali mwaka wa 2022.

“Wakati huo utakapofika, nitajua ni nani nitaunga mkono, lakini sina mpango wa kuwania kiti cha ugavana,” alisema.

Haya yalitokea wiki moja baada ya, Spika wa Garissa kubahatika baada ya madiwani wa eneo hilo kuondoa hoja ya kumuondoa bungeni.

MCAs wakiongozwa na mwenzao Mohamud Aden walikuwa wamewasilisha hoja ya kumshtaki spika akimtuhumu kwa ukiukaji mkubwa wa katiba.

Walakini, gavana Korane alilazimika kupatanisha madiwani hao akilaumu vikali wanasiasa wa eneo hilo kwa “kuleta ugomvi kwa mambo yasiyo na maana”.

Alimtaja Bw Duale kuwa miongoni mwa wanasiasa hao.

You can share this post!

Mavuno ya mahindi kupungua – utafiti

Uhasama wa kisiasa wa Sang na Cherargei wazuka tena mbele...