• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Faini Sh10,000 au jela kutema mate jijini

Faini Sh10,000 au jela kutema mate jijini

Na COLLINS OMULO

UTATOZWA faini ya Sh10,000 au kutupwa jela kwa miezi sita kwa kupenga kamasi bila kitambaa au karatasi ya shashi, au kutema mate barabarani, jijini Nairobi.

Aidha, kuishi au kulala jikoni au katika chumba ambamo chakula huandaliwa kutavutia faini isiyozidi Sh50,000, kifungo cha miezi sita gerezani au yote mawili huku kurudia kwa makosa hayo baadaye kukitozwa faini isiyopungua Sh100,000 au kifungo cha jela kwa muda usiozidi miezi 12 au yote mawili.

Mabadiliko haya mapya yamejiri baada ya Kaimu Gavana wa Nairobi Ann Kananu kutia saini kuwa sheria Mswada wa Kaunti ya Jiji la Nairobi kuhusu Usumbufu kwa Umma 2020.

Sheria hiyo mpya imeanzisha kundi jipya la kanuni na masharti mapya yanayolenga kudumisha usafi katika jiji kuu kwa kudhibiti masuala ambayo ni kero kwa umma.

Mswada huo uliopitishwa na Bunge la Kaunti hiyo mnamo Septemba 2020, uliwasilishwa na Diwani wa Riruta, James Kiriba.

Miongoni mwa sheria hizo mpya ni pamoja na kukojoa katika sehemu zisizofaa, kujipatia riziki kimaksudi kutokana na mapato ya ukahaba, kumwaga maji machafu, majitaka au mafuta barabarani au kwenye chemichemi za maji, na kuweka vizuizi njiani.

Sheria hiyo vilevile imepiga marufuku wakazi kuruhusu miti kwenye makao yao au sehemu za kazi kufunga barabara au sehemu za watu kutembelea, huku ikiwa ni hatia kuendesha pikipiki au gari kwenye maeneo ya watu kupitia, kucheza muziki kwa sauti ya juu na kuvuta sigara katika sehemu ambazo hazijatengwa.

Kuendesha pikipiki au gari kwenye sehemu za watu kupitia sasa kutachukuliwa kama kero kwa umma na hatia kwenye barabara na mitaa ya umma.

Wakati huo huo, kwenda haja kubwa au haja ndogo barabarani au katika sehemu yoyote iliyo wazi ikiwemo kuwasha moto katika barabara au mtaa wa umma bila idhini kutoka kwa katibu wa kaunti, sasa ni hatia.

Aidha, itachukuliwa kama hatia kuacha mbwa unayefuga kurandaranda barabarani au kwenye mitaa ya umma, kuosha, kuunda au kuharibu gari yoyote jijini, isipokuwa katika hali za dharura, kuvuta sigara katika sehemu za umma na kondakta kung’ang’ania abiria.

You can share this post!

Walimu wakosa chanjo ya corona kituoni

Ruto aidhinisha Ngirici kwa kiti cha ugavana Kirinyaga