• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:07 PM
Familia 100 zapiga hesabu upya baada ya kuhamishwa pahala walipoishi tangu 1986

Familia 100 zapiga hesabu upya baada ya kuhamishwa pahala walipoishi tangu 1986

NA SAMMY KIMATU

FAMILIA zaidi ya 100 zimeanza kuondoka kutoka kwa makazi yao baada ya korti kuagiza zihame kutoka kwa ardhi mali ya mtu binafsi.

Naibu kamishna wa kaunti ndogo ya Starehe, Bw John Kisang aliambia Taifa Leo kwamba wakazi hao katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Fuata Nyayo, tarafa ya South B walikuwa wakiishi kwa ardhi ya mwenyewe tangu 1986.

Alifafanua kwamba sehemu hiyo ya ardhi iliyo mkabala wa barabara ya Aoko hatua chache kutoka kwa kanisa la ACK St Veronicah.

Aidha, aliongeza kwamba wakazi hao walipewa ilani ya kuondoka baada ya korti kuagiza waondoke mnamo Mei 2023.

“Licha ya kupewa siku saba katika notisi iliyopeanwa na korti mnamo Mei walipopewa muda wa wiki moja kujibomolea nyumba zao wenyewe, walidinda,” Bw Kisang akasema.

Asubuhi ya leo Alhamisi, Taifa Leo imewapata baadhi yao wakibomoa nyumba za mawe na wengine wakibomoa zilizojengwa kwa mabati.

“Kulikuwa na nyumba za orofa zilizojengwa kwa mabati na zingine kujengwa kwa mawe. Walikuwa pia na nyumba za mawe walikofanyia biashara kando ya barabara ya Aoko,” Bw Tito Muvengei, aliye mwenyekiti wa mtaa huo, akawaambia wanahabari.

Kwa mujibu wa mkuu wa tarafa ya South B, Bw Solomon Muraguri, ardhi hiyo inamilikiwa na Kabur Saghani na ndugu wake.

“Wakazi waliitwa katika mkutano wa kujadiliana pamoja ulioongozwa na Sanghani kupitia kwa ofisi yangu,” amesema Bw Muraguri.

Isitoshe, afisa huyo wa utawala ameambia Taifa Leo kwamba kabla ya notisi ya kuhama kutolewa, wakazi walipewa nafasi kusema ikiwa wako tayari kununua ardhi yenyewe kwa hiari yao bora atakayenunua alipe Sh200 milioni.

“Wakazi walipewa ofa ya Sh200 milioni kwa yeyote aliyetaka kununua ardhi hiyo kabla ya kuondoka katika shamba hilo lakini walishindwa. Ndipo sasa imebainika hawana chaguo jingine ila kuhama,” Bw Muraguri akaongeza.

Bw Muraguri aliongeza kwamba watu hao walikuwa wamejenga nyumba za kudumu bila idhini ya serikali kinyume cha sheria kuanzia mwaka 1987 wakati kesi ilipelekwa mahakamani.

Vilevile, Muraguri alifafanua kwamba tofauti na hapo awali ambapo tingatinga zilikuwa zikibomoa nyumba wakati watu wakifurushwa, raundi hii, wakazi wanapewa notisi kujibomolea nyumba na kutoa mali yao kwa taratibu.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Ezra Chiloba ajiuzulu kutoka wadhifa wake wa Mkurugenzi...

Kutana na ‘beach boy’ mkongwe zaidi Lamu

T L