• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 6:55 AM
Familia ya hayati yammiminia sifa kwa malezi bora

Familia ya hayati yammiminia sifa kwa malezi bora

NA WINNIE ONYANDO

FAMILIA ya hayati Rais Mstaafu, Mwai Kibaki, Jumamosi ilimmiminia sifa tele ikisema hakutelekeza wajibu wake kama mzazi nyumbani.

Ikiongozwa na Jimmy Kibaki, familia ilimsifu na kusema kuwa mbali na kuwa rais, alikuwa mzazi ambaye alipenda familia yake na kutenga muda wa kukaa nayo.

“Japo alikuwa kiongozi anayeheshimika nchini, alikuwa baba na alitupenda sana. Alitutengea muda na kuhakikisha kuwa tunapata mahitaji yetu yote. Ninampenda kama baba na daima atabaki moyoni mwangu,” akasema Bw Jimmy.

Alisema kuwa baba yake alimtaka awe shupavu na msomi kama yeye.

“Kila mara alikuwa akifuatilia matokeo yangu. Ninakumbuka kuna wakati nikiwa katika kidato cha pili na matokeo yangu hayakuwa mazuri. Aliniambia nimchungie mifugo na awe akinilipa kwa kazi hiyo. Huo ndio wakati nilipoamua kutia bidii masomoni,” akasema Jimmy.

Kwa upande mwingine, alisema kuwa babake alikuwa kielelezo kwake na kila mara alimwongoza kwa upole na kumshauri atie bidii katika kila jambo.

Kwa upande wake, Judy Wanjiku Kibaki alimtaja babake kama kiongozi aliyewapenda na kuwaenzi.

Alisema babake alikuwa akimpeleka shuleni kila asubuhi na hata kuhudhuria mikutano ya maendeleo shuleni kama wazazi wengine.

“Alituonyesha upendo bila upendeleo. Alienzi elimu sana. Kila mara angetushauri tusome kwa bidii na kufuata ndoto zetu. Alinifunza mengi na kila mara nilikuwa nikimtazamia,” akasema Bi Wanjiku.

Alimsifu babake kwa kutomlazimisha kuingia kwenye siasa na kuanika maisha yake kwa umma.

Kadhalika, alisema amejifunza subira kutoka kwa hayati babake ambaye alionyesha sifa ya kuwa mtulivu wakati wote.

“Katika uongozi wake, alikuwa mtulivu na mpenda amani. Hata wakati wa siasa, alikuwa mwenye subira na kila mara angehubiri amani. Daima atabaki kwenye kumbukumbu zetu,” akasema Bi Wanjiku.

Jimmy Kairu, rafiki wa dhati wa familia ya hayati Mzee Kibaki alisema kuwa daima uhusiano wa familia hizo mbili utabaki kidete.

Alisema kuwa familia hizo mbili zimekuwa zikishirikiana kwa karibu na kuwa kamwe uhusiano huo hautafifia.

Alimtaja Mzee Kibaki kama kiongozi ambaye nia yake kuu ilikuwa ni kuendeleza uchumi na kuwaunganisha Wakenya.

  • Tags

You can share this post!

Liverpool wakomoa Newcastle na kuweka hai matumaini ya...

Kibaki azikwa kwa heshima za kijeshi

T L