• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Familia yaidhinishwa kumiliki ardhi ya Sh2b

Familia yaidhinishwa kumiliki ardhi ya Sh2b

SIAGO CECE na BRIAN OCHARO

FAMILIA moja katika Kaunti ya Kwale, hatimaye imepata idhini rasmi kutoka kwa serikali kuu kumiliki ardhi ya ukubwa wa ekari 289 katika Kisiwa cha Wasini.

Familia ya Saggaf imekuwa ikipigania umiliki wa ardhi hiyo ambayo thamani yake imekadiriwa kuzidi Sh2 bilioni kwa zaidi ya miaka 30.

Naibu Kamishna wa Kaunti anayesimamia Lunga Lunga, Bw Alason Hussein, aliongoza maafisa wa usalama na masoroveya kufanya ukaguzi wao kwenye kipande hicho cha ardhi.

Usoroveya ulikuwa umekwama zaidi ya mara tatu kufuatia malalamishi ya baadhi ya wakazi wa eneo hilo lakini hatimaye shughuli hiyo ikakamilishwa wiki iliyopita.

“Tumefurahi kuwa shughuli hiyo ilifanywa. Sasa tunatazamia kupata hatimiliki ya ardhi hiyo,” akasema msemaji wa familia, Bw Mohamed Maula.

Hatua ya kufanya usoroveya ilichukuliwa baada ya Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) kuamua ardhi hiyo irudishwe kwa familia ya Saggaf Alawys, ikisema walitendewa dhuluma za kihistoria kwa kuishi kama maskwota ilhali wanamiliki ardhi inayozozaniwa.

Warithi wa ardhi hiyo ni watoto wa Saggaf ambao ni Hassan Nassir, Mohamed Nassir na Ahmed Nassir.

Watu kwenye kikundi, walielekea mahakamani kudai umiliki wa ardhi hiyo lakini Mahakama Kuu ikaamua katika mwaka wa 2015 kuwa familia ya Saggaf ndio wamiliki halali.

Familia hiyo ililaumu wanyakuzi wa ardhi kwa kupuuza agizo hilo na kujaribu kuwapokonya sehemu hiyo ambayo ni kubwa mno katika Kisiwa cha Wasini.

Wakazi walilalamika kuwa, usoroveya ulifanywa usiku na hivyo basi wakatilia shaka uhalali wake.

Malalamishi sawa na hayo yalitolewa pia na Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya ambaye wiki iliyopita alituliza hamaki ya wakazi waliojitokeza kuzuia usoroveya kufanywa.

“Sijawahi kusikia ardhi ikifanyiwa usoroveya muda kama huo. Hii inamaanisha shughuli hiyo nzima ilikuwa haramu. Haki za wakazi zinafaa kupewa kipaumbele,” akasema.

Hata hivyo, Bw Maula alisema sehemu ya ardhi ambayo imerudishwa kwa familia yao haina wakazi wowote wanaoishi isipokuwa wawekezaji waliokuwa wameanza kujenga hoteli za kifahari.

Aliwaondolea wakazi wanaopakana na ardhi yao hofu kwamba watafurushwa.

You can share this post!

Jumwa adai serikali ya Kingi haijali wakazi

Hofu muda wa NMS ukielekea kumalizika