• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:09 AM
Hofu muda wa NMS ukielekea kumalizika

Hofu muda wa NMS ukielekea kumalizika

Na COLLINS OMULO

HOFU imeibuka kuhusu ikiwa Halmashauri ya Kusimamia Jiji (NMS) itaongezewa muda kuendelea kuhudumu jijini Nairobi, baada ya kipindi chake kukamilika.

Halmashauri hiyo ilikuwa imepewa muda wa miaka miwili kusimamia baadhi ya sekta muhimu jijini, ambapo sasa imebaki miezi sita pekee kipindi hicho kukamilika.

Madiwani katika Kaunti ya Nairobi wanaonekana kugawanyika kuhusu ikiwa halmashauri inapaswa kuongezewa muda zaidi.

Muda wa kuhudumu wa halmashauri utakamilika rasmi mnamo Machi 18, 2022.

Kando na hayo, wataalamu na wadadisi wa masuala ya sheria wameonya dhidi ya kuongeza muda wa taasisi hiyo.

Wanasema hatua hiyo haitakuwa rahisi, kwani huenda ikapingwa kupitia mahakama.

NMS ilibuniwa na Serikali ya Kitaifa kuisaidia serikali ya kaunti kuendesha baadhi ya miradi na sekta muhimu zilizoonekana kuishinda serikali ya aliyekuwa gavana wa Nairobi, Mike Sonko.

Mdahalo huo uliibuka Jumanne wiki iliyopita, baada ya diwani James Kiriba (Riruta) kuwasilisha hoja ya kubuniwa kwa kamati maalum itakayosimamia mchakato wa kurejesha usimamizi wa sekta nne muhimu zilizochukuliwa na NMS kwa serikali ya kaunti.

NMS ilibuniwa mnamo Februari 2020, baada ya Bw Sonko na aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi, Eugene Wamalwa, kutia saini mkataba huo chini ya usimamizi wa Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi.

Baadhi ya sekta zilizochukuliwa na halmashauri hiyo ni usimamizi wa sekta ya afya, huduma za uchukuzi, masuala ya mipango na ustawishaji wa jiji.

Kulingana na Bw Kiriba, mkataba huo uliipa NMS muda wa miaka miwili kusimamia sekta hizo.

Alisema kuwa kulingana na mkataba huo, muda wa halmashauri hiyo unapaswa kukamilika Machi 2022.

Hata hivyo, baadhi ya madiwani wanaonekana kupinga msimamo huo.

Siku moja baada ya kuwasilisha hoja hiyo, Kiranja wa Wengi Paul Kados alimwandikia barua Spika Benson Mutura, kumfahamisha Chama cha Jubilee (JP) kimeanza hatua za kumwadhibu Bw Kiriba.

Kiongozi wa Chama wa Mawakili Kenya (LSK), Nelson Havi, anasema itakuwa ukiukaji wa Katiba kuongeza muda wa kuhudumu wa NMS.

“Hakutakuwa na sababu yoyote halisi kuiongezea muda NMS. Kisheria, muda wake unapaswa kulingana na mwisho wa kipindi cha kuhudumu cha Bw Sonko kama gavana. Hata hivyo, najua huenda wakaongeza muda huo,” akasema Bw Havi.

Ni kauli sawa zinazotolewa na mawakili Steve Ogolla na Bobby Mkangi.

You can share this post!

Familia yaidhinishwa kumiliki ardhi ya Sh2b

WASONGA: Chiloba, wenzake wasaidie IEBC kufanikisha kura...