• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Jumwa adai serikali ya Kingi haijali wakazi

Jumwa adai serikali ya Kingi haijali wakazi

ALEX KALAMA na VALENTINE OBARA

MBUNGE wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, ameisuta Serikali ya Kaunti ya Kilifi akidai kuwa haitilii maanani mahitaji muhimu ya umma.

Bi Jumwa ambaye anatarajiwa kuwania ugavana mwaka 2022 kupitia Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Naibu Rais William Ruto, alisema kaunti hiyo inayoongozwa na Gavana Amason Kingi, inafaa kuangazia zaidi masuala ya kufaidi wananchi katika bajeti zake.

Kulingana naye, asilimia kubwa ya masuala yaliyojumuishwa katika bajeti ya serikali ya Kaunti mwaka huu 2021, inawanufaisha viongozi na wala si wananchi.

“Matatizo ya mwananchi wa kawaida hayaangaziwi kwenye bajeti ya Kaunti hii ya Kilifi. Badala yake bajeti hiyo huangazia sana masuala ya kuwanufaisha viongozi,” akadai Bi Jumwa.

Alipigia debe azimio lake la kuwania ugavana wa kaunti hiyo mwaka 2022, akiahidi kuwa endapo ataibuka mshindi uchaguzini atahakikisha bajeti ya kaunti itamuangazia mwananchi wa kawaida mashinani.

Mbunge huyo aliyeasi Chama cha ODM, alitaja hatua ya kuwepo kwa huduma duni na ukosefu wa vifaa vya matibabu katika vituo vya afya Kaunti ya Kilifi, kama mifano ya matatizo ambayo yanaendelea kuwakumba wananchi katika kaunti hiyo.

Katika miezi ya hivi majuzi, kumekuwa na malalamishi miongoni mwa wakazi na baadhi ya viongozi kuhusu huduma duni za afya katika kaunti hiyo, na vile vile ukosefu wa hatua mwafaka kuhusu janga la njaa linalokumba sehemu mbalimbali za kaunti.

Baadhi ya maafisa katika kaunti wamewahi kukiri kumekuwa na changamoto katika juhudi za kuimarisha utoaji huduma za afya hasa wakati wa janga la corona kwa vile inashukiwa pesa zilizotengewa idara ya afya zilifujwa.

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) inaendeleza uchunguzi kuhusu suala hilo.

“Hapa katika Kaunti ya Kilifi vituo vingi vya afya vinakosa vifaa vya matibabu. Haya ni baadhi ya matatizo yanayomwandama mwananchi wa kawaida,” alisema Bi Jumwa.

Wakati huo huo, aliwasuta baadhi ya viongozi waliokuwa wakiunga mkono marekebisho ya Katiba kupitia kwa Mpango wa Maridhiano (BBI) katika Kaunti ya Kilifi.

Mbunge huyo alisema kuwa mchakato wa BBI haukuwa na nia yoyote ya kumfaidi mwananchi wa kawaida na badala yake ingemkandamiza kwa kumkosesha huduma bora anazopaswa kupata.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki, aliwasilisha malalamishi katika Mahakama ya Juu dhidi ya uamuzi wa Mahakama ya Rufaa ambao uliharamisha urekebishaji wa Katiba kupitia kwa BBI.

Hatua hiyo ni ya mwisho kujaribu kufufua marekebisho ya Katiba kwani mchakato huo ulikuwa pia umeharamishwa na majaji wa Mahakama Kuu.

Dkt Ruto na wandani wake wamezidi kupinga jaribio la kufufua BBI wakisisitiza kuwa mpango huo hauna manufaa kwa wananchi wa kawaida, bali utaleta mzigo mzito wa kugharamia mishahara na marupurupu ya ongezeko la viongozi wa kisiasa akiwemo waziri mkuu na manaibu wake wawili.

You can share this post!

Kioja mama akiuza shamba aponde raha

Familia yaidhinishwa kumiliki ardhi ya Sh2b