• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Familia zaidi ya 100 zapoteza nyumba zao baada ya moto kuteketeza nyumba 150 mtaani Mukuru-Kayaba

Familia zaidi ya 100 zapoteza nyumba zao baada ya moto kuteketeza nyumba 150 mtaani Mukuru-Kayaba

Na SAMMY KIMATU

ZAIDI Ya familia mia moja zimepoteza nyumba zao baada ya moto mkubwa kuteketeza nyumba 150 katika mtaa mmoja wa mabanda katika Kaunti ya Nairobi.

Kisa hicho kilitokea mwendo wa saa nne za mchana katika eneo la Kambi Moto, mtaani wa mabanda wa Kayaba ulioko katika kaunti ndogo ya Starehe mnamo Alhamisi.

Kwa mujibu wa kiongozi wa Vijana tarafa ya South B, Bw Rodriques Lunalo, moto ulianzia ndani ya nyumba moja kabla ya kuenea kwa nyumba zingine.

Inadaiwa kuwa mwenye nyumba, ambaye ni mama alikuwa amewacha mtungi wa gesi akipika chakula na kuondoka nyumbani kabla ya kuzima gesi.

“Kabla ya moto wa leo, usiku wa kuamkia leo majirani walizima moto mwingine kabla ya kuenea baada ya mtungi wa gesi kuwaka mkazi akiendelea na mapishi. Nimeweza kuondoa mitungi tano ya gesi wakati tukipambana kuuzima moto wa leo,’’ Bw Lunalo asema.

Fauka ya kuwa mkasa huo ulitokea wakazi wengi wakiwa kazini, Bw Lunalo aliwaongoza vijana kutoka mtaa wa Kayaba, Hazina na Sokoni kuungana pamoja kuzima moto.

Kutokana na ukosefu wa barabara ya kuingia kwenye eneo la mkasa, vijana walilazimika kubomoa baadhi ya nyumba ili kuzuia moto kusambaa zaidi.

Wakati mmoja, vijana waliojawa na gadhabu ya gari la kuzimamoto kuingia mtaani, waliwarushia mawe maafisa wa kuzima moto kutoka serikali ya Kaunti ya Nairobi ndiposa wapore mali.

Chifu wa Landi Mawe, Bw Mulandi Kikuvi alikikashifu kitendo cha vijana kupinga maafisa wa kaunti kuzima moto na kuongeza kwamba kitendo hicho kimepitwa na wakati.

“Nimethibitisha afisa mmoja wa kuzima moto amepigwa mawe na kujeruhiwa mguuni wake wa kushoto. Pia bomba la kupitisha maji ilikuwa imekatwa kwa panga ili maji yasifike kwenye eneo la mkasa,” chifu Mulandi akasema.

Kabla ya kuwasili kwa lori la kuzima moto, vijana walipanga foleni kuanzia mto Ngong hadi kwenye mkasa wakijihami kwa beseni na mitungi ya kuchota maji.

Wengine nao walivunja paipu za kusambaza maji mtaani na kutumia maji yake kuzima moto.

Eneo la mkasa ilikuwa ni pahali palipojengwa nyumba za kukodisha na zilizokuwa zote zimejengwa kwa mabati.

Vilevile, hakuna vibanda vya biashara vilyokuwa kwenye maeneo hayo.

  • Tags

You can share this post!

Vijana wahimizwa kuzingatia teknolojia ya Ajira Digital...

Polisi watwaa daraja lililoibwa kutoka Mukuru-Kayaba