• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:55 PM
Vijana wahimizwa kuzingatia teknolojia ya Ajira Digital Kenya

Vijana wahimizwa kuzingatia teknolojia ya Ajira Digital Kenya

Na LAWRENCE ONGARO

VIJANA wamehimizwa kuzingatia utumizi wa mitandao ya kidijitali aina ya Ajira Digital Kenya, ili kujiendeleza kimaisha.

Waziri wa Habari na Teknolojia (ICT), Bw Joe Mucheru, ametoa changamoto kwa vijana popote walipo kujitokeza kuingilia mpango huo.

Naibu katibu katika wizara hiyo Bi Lucy Malili, alisoma hotuba ya Mucheru alipozuru Chuo Kikuu cha Zetech katika mji wa Ruiru.

Kulingana na hotuba ya waziri, vijana walishauriwa kukumbatia mpango huo wa Ajira Digital Kenya, ili kupata njia ya kujikimu kimaisha kupitia mtandao.

Alieleza kuwa serikali ilikuwa ikitarajia kuweka vituo vya kuhamasisha vijana kuhusu Ajira Digital.

Imedaiwa kuwa vijana wengi wamenufaika pakubwa kutokana na mpango huo na kwa hivyo ni muhimu wakihusishwa vilivyo.

“Mpango huo ni muhimu kwa sababu unaendesha mambo yako mahali popote ulipo hata kwenye nyumba,” Waziri alieleza katika hotuba yake.

Kulingana na waziri huyo, serikali imejitolea kuona ya kwamba asilimia kubwa ya vijana wanajitegemea baada ya kukamilisha masomo yao vyuoni.

Bi Malili naye alieleza kuwa serikali itashirikiana na chuo cha Zetech kuona ya kwamba inapata kituo cha Ajira Digital ili kufunza watu jinsi ya kutumia mitandao.

Alieleza kuwa mpango huo utakuwa bila malipo na kwa hivyo watu wengi wamehimizwa kujitokeza.

“Ajira Digital ni mwelekeo mzuri kwa vijana wanaotafuta ajira na masomo hayo ni ya bure. Kwa hivyo tunawahimiza vijana wengi wajitokeze kujifunza,” alifafanua Bi Malili.

Naibu chansela wa Zetech Prof Njenga Munene alieleza walibuni Ajira Digital Kenya mwaka wa 2018 kwa lengo la kuwahamasisha wanafunzi jinsi ya kujitegemea.

Alisema mpango huo umesaidia wanafunzi wengi ambao sasa wamejiajiri wenyewe kupitia mtandao wa Ajira Digital.

Prof Munene alitoa mwito kwa wizara kuja na mikakati mipya ili kuona ya kwamba vijana wengi wananufaika na mradi huo.

Alieleza kuwa mji wa Ruiru ni mojawapo ya kaunti ndogo zenye idadi kubwa ya wakazi na kwa hivyo ni vyema serikali kuangazia mipango yake hapo.

Alitoa mwito kwa serikali iwape miradi tofauti katika chuo hicho cha Zetech ili vijana wenye ujuzi wazidi kufunza wanafunzi wengine ili wawe na ujuzi.

Bw Kamau Wa Njuguna ambaye ni mwanafunzi mwenye ujuzi wa Ajira Digital alikiri mradi huo umenufaisha watu wengi.

“Jinsi tunavyoelekea katika enzi za kidijitali ni muhimu vijana wengi wajitokeze ili wapate mafunzo jinsi ya kujitegemea,” alisema Bw Njuguna.

Alitoa changamoto kwa vijana kujitokeza kwa wingi kuona ya kwamba wanakuwa wabunifu kwa kujitafutia ajira kupitia Ajira Digital.

  • Tags

You can share this post!

Leopards na Gor Mahia kuumizana fainali ya Betway Cup Julai...

Familia zaidi ya 100 zapoteza nyumba zao baada ya moto...