• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Hakuna kuvalia ‘crocs’ wakati wa shughuli rasmi za masomo chuoni MMUST

Hakuna kuvalia ‘crocs’ wakati wa shughuli rasmi za masomo chuoni MMUST

NA FRIDAH OKACHI

WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro (MMUST) hawataruhusiwa kuvalia mavazi mafupi, nguo za mtindo mraruko, viatu vya plastiki, viatu aina ya crocs, na mtindo wa tumbo cut wakati wa shughuli rasmi za masomo chuoni.

Usimamizi wa chuo hicho umewaonya wanafunzi dhidi ya kuvalia mavazi hayo ukisema kuwa mavazi hayo hayana heshima.

Marufuku ya mavazi hayo yanalenga wanafunzi wa kike sawia na wa kiume.

Kulingana na memo iliyosambazwa kwa wanafunzi, Mkuu wa Maslahi ya Wanafunzi Kwenye Taasisi hiyo Bernardatte Abwao aliibua wasiwasi wa mavazi yanayovaliwa na wanafunzi na kuyataja yasiyo ya heshima.

“Nachukua fursa hii kuwapongeza wanafunzi wote wanaovalia nadhifu wakija kwenye chuo hiki. Hata hivyo, tumeona kuwa wengine wanavalia visivyo,” aliandika kwenye memo.

Chuo hicho kimepiga marufuku wanafunzi kuvalia mashati-tao yenye maandishi na lugha chafu, viatu aina ya crocs na viatu vyote vya plastiki.

Katika barua hiyo vilevile amewaonya akina dada wenye mazoea ya kuvalia mavazi yanayoonyesha baadhi ya sehemu zinazofaa kufichwa kwa kawaida, sidiria ambazo hazina kamba na suruali fupi kupindukia.

Chuo hicho kimeeleza kuwa aina yote ya mavazi yaliyotajwa hayaambatani na maadili ya shule hiyo.

Kwa upande wa jinsia ya kiume, wamekatazwa kuvalia suruali ndefu ambazo hazifiki kwenye kiuno yaani sagging trousers na nguo zinazoonyesha kifua.

Pia wanafunzi wa kiume hawatakiwi kutoboa sehemu za mwili pamoja na kuweka nywele ndefu almaarufu dreadlocks.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yakatiza mkataba na madaktari wa Cuba

Wataalamu waonya bei ya unga itaendelea kupanda

T L