• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Wataalamu waonya bei ya unga itaendelea kupanda

Wataalamu waonya bei ya unga itaendelea kupanda

STANLEY KIMUGE na BARNABAS BII

WATAALAMU wa Masuala ya Kilimo wameibua wasiwasi kuhusu kuendelea kupanda kwa bei ya unga licha ya serikali kupiga marufuku uagizaji wa mahindi kutoka nje ya nchi.

Serikali ilichukua hatua hiyo ili kuwazuia wakulima kupata hasara kwa sababu mahindi ambayo huagizwa nje ya nchi hujaa sokoni na kufanya bei kushuka kwa kiwango kikubwa.

Kwa mujibu wa wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti ya Tegemeo, bei ya mahindi na pia unga itaendelea kuwa ghali kutokana na hitaji kubwa sokoni.

Dkt Timothy Njagi kutoka Taasisi ya Tegemeo, alisema kuwa licha ya bei kudhibitiwa kimataifa, baadhi ya kampuni za kusaga mahindi, hazitaki kuagiza mazao hayo kutokana na thamani ya shilingi ya Kenya kudorora dhidi ya dola ya Amerika.

“Bei ya mahindi ilishuka katika soko la kimataifa kutoka Sh56, 677 kwa tani moja hadi Sh34, 304 kutokana na hatua ya Ukraine kujaza mahindi tele kwenye soko la Ulimwenguni. Kwa kuwa thamani ya shilingi ya Kenya inafanya vibaya ikilinganishwa na dola, bei ya mahindi itaendelea kuwa ghali,” akasema Dkt Njagi.

Japo marufuku ya uagizaji wa mahindi kutoka nje iliwekwa kuwasaidia wakulima kuyauza mahindi yao kwa bei bora, bado unga unanunuliwa kwa bei ya juu na kufanya familia nyingi kuumia.

“Marufuku ya uagizaji mahindi na ngano itawanufaisha wakulima. Hata hivyo, wanunuzi nao wataendelea kulipa pesa za juu kwa unga, “ akaongeza Dkt Njagi huku akitaka serikali iibuke na mikakati ya kukinga wanunuzi.

Wiki iliyopita, Rais William Ruto alisitisha kutolewa kwa vyeti vya kuagiza mahindi na ngano, akilenga kuwanusuru wakulima.

Rais alisema uamuzi huo utabadilishwa tu pale Kenya itaanza kukabiliwa na ukosefu wa chakula.

Kwa sasa unga wa pakiti ya kilo mbili unauzwa kwa kati ya Sh180-Sh200. Gunia la kilo 90 la mahindi nalo linauzwa kwa kati ya Sh3,800-Sh4,200.

Nchini Uganda, gunia la kilo 90 ni Sh4,350 huku likiuzwa Sh4,500 Tanzania.

Kaskazini mwa Bonde la Ufa kampuni kama AFEX sasa inalenga kununua magunia milioni mbili kutoka kwa wakulima msimu huu.

Kenya nayo inalenga kuvuna magunia milioni 44 ya mahindi huku ukanda wa Kaskazini mwa Bonde la Ufa ukitarajiwa kutoa magunia milioni 23.

Kwenye idadi hiyo, Kaunti ya Trans Nzoia inatarajiwa kutoa magunia milioni saba huku Uasin Gishu ikitoa magunia milioni sita.

  • Tags

You can share this post!

Hakuna kuvalia ‘crocs’ wakati wa shughuli rasmi...

Aliyeacha masomo kukimbilia pesa za haraka machimboni asema...

T L