• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:07 PM
Hofu Ulaya ikipunguza chanjo za Covid-19 Afrika

Hofu Ulaya ikipunguza chanjo za Covid-19 Afrika

Na PAULINE KAIRU

KUMEZUKA hali ya wasiwasi barani Afrika kuhusu kupungua kwa idadi ya chanjo za virusi vya corona, baada ya serikali kadhaa za nchi za Ulaya kusema zitaanza kuwapa tena raia wake chanjo hizo.

Hii ni licha ya idadi kubwa ya raia hao kupewa chanjo hizo kwa awamu za kwanza na pili.Serikali zilisema zinalenga kuboresha kiwango cha chanjo ambazo raia hao walipata ili kuwawezesha kukabili makali ya virusi hivyo ikiwa wataambukizwa.

Imeibuka mataifa hayo yanaagiza chanjo aina ya Johnson & Johnson kutoka kampuni ya Aspen Pharmacare kutoka Afrika Kusini, iliyopewa kibali cha kutengeneza chanjo hizo majuzi ili kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na uhaba uliopo.

Kwa sasa, Afrika bado inakabiliwa na uhaba mkubwa wa chanjo hizo, licha ya misaada inayoendelea kutolewa kupitia mpango wa Covax na nchi za Magharibi.

Wanaharakati wa afya barani Afrika wamekasirishwa vikali na tangazo la aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, kwamba taifa hilo linapanga kuagiza dozi milioni kumi kutoka kwa kampuni ya Aspen.

Brown alitoa kauli hiyo kwenye makala aliyoandika katika gazeti la ‘The Guardian’ mapema wiki hii.Chanzo cha ghadhabu hiyo ni kuhusu sababu ya mataifa hayo kuagiza chanjo kutoka Afrika, ilhali idadi kubwa ya raia wake wamechanjwa dhidi ya virusi hivyo.

Brown alisema chanjo hizo zimepangiwa kusafirishwa barani Ulaya katika miezi ya Agosti na Septemba.Kufikia Ijumaa, takwimu zilionyesha asilimia 87.3 ya raia wa Uingereza washapokea awamu ya kwanza ya chanjo hizo huku asilimia 75.7 wakiwa washapokea chanjo kwa awamu ya pili.

Hii ni ikilinganishwa na Afrika, ambapo kati ya watu 1.3 bilioni, ni asilimia 1.8 pekee ambao wamepokea chanjo hizo.

Kufuatia tangazo hilo, kumezuka maandamano makubwa nchini Afrika Kusini, raia wakiishinikiza serikali ya taifa hilo kueleza wazi mkataba uliopo kati yake na kampuni zinazotengeneza chanjo ya Johnson & Johnson na aina zingine.Walitishia kuchukua hatua za kisheria ikiwa haitaweka wazi makubaliano hayo.

Kampuni ya Aspen ilipewa kibali hicho kufuatia idadi ndogo ya chanjo ambazo zinatolewa kwa nchi za Afrika na Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia mpango wa Covax.

Hapo jana, Mkurugenzi wa WHO barani Afrika, Dkt Matshidiso Moseti alisema: “Wakati juhudi zetu zilionekana kuanza kupata mafanikio, vikwazo vipya vinatuandama. Baadhi ya nchi tajiri zinaendelea kuficha chanjo, hali inayovuruga juhudi zote za usawa kwenye utoaji wake. Karibu raia wote wamepata chanjo katika nchi hizo ikilinganishwa na Afrika ambapo ni watu sita pekee kati ya 100 ambao wamepata.”

You can share this post!

Wadau wateta kampuni ya Joho kupewa kandarasi

Hatujaunga mkono Raila wala Ruto – Viongozi Mlima...