• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Idara yaonya kuhusu wahubiri bandia Kilifi

Idara yaonya kuhusu wahubiri bandia Kilifi

Na MAUREEN ONGALA

IDARA ya watoto katika Kaunti ya Kilifi, imetoa tahadhari kuhusu ongezeko la visa ambapo wazazi huwapeleka watoto waombewe wanapougua badala ya kuwapeleka hospitalini.

Maafisa wa idara hiyo wanaamini kuwa hali hiyo imechangiwa na ongezeko la wahubiri wanaodai kuwa na nguvu za kuponya magonjwa mbalimbali eneo hilo.

Wazazi wakati mwingi hushawishika kuwapeleka watoto waombewe kwa vile wahubiri huwaambia kwamba wamerogwa na watu wanaodaiwa kuwa ni wachawi.

Eneo la Kilifi ni miongoni mwa mengine nchini ambapo suala la uchawi limekita mizizi.

Mshirikishi wa masuala ya watoto katika kaunti hiyo, Bw George Migosi, alisema mienendo hii imechangia pia kuvunja ndoa kwani wazazi hukosa kuelewana wakati mmoja anapotaka mtoto atibiwe hospitalini, na mwingine hutaka apelekwe kwa maombi.

Alionya wahubiri aina hiyo kwamba wataanza kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Tumekuwa na changamoto kubwa ambayo imezidi kuathiri afya ya watoto. Hawapati matibabu bora kwa sababu wazazi hawataki kuwapeleka hospitalini wakifuata imani potovu,” akasema.

Bw Migosi alisema kuwa wahubiri hao wenye imani potovu huwahadaa wazazi hata kususia kuwapeleka watoto wao kupata chanjo muhimu zinazotolewa na serikali kuwakinga dhidi ya magonjwa hatari.

Wakati mwingine, huwa inawalazimu maafisa ya idara ya watoto kuwachukulia hatua za kisheria wazazi hao.

“Wazazi wengi husema kuwa kuna mwombaji mahali fulani ambaye huwa wanapeleka watoto wakiwa wagonjwa. Wengine hata huzidiwa na ugonjwa na kufa,” akasema.

Alisema wagonjwa wanastahili kushughulikiwa katika kituo cha afya kinachotambulika na wizara ya afya wala sio katika makanisa ya uongo na majumbani mwa wahubiri.

“Watoto hawajui kutofautisha jambo baya na zuri, na hii ndio sababu wanalindwa na sheria. Wakipata mtu mzima anayetaka kuwapotosha, watamfuata bila kujua wanachofanya,” akasema Bw Migosi.

Alitoa mfano wa kanisa moja maarufu eneo la Malindi ambapo mhubiri aliwahi kukamatwa na kushtakiwa kwa kuwakataza wazazi kuwapeleka shuleni na hospitalini.

Kulingana naye, mhubiri huyo alitoa mafunzo ya kupotosha ya kidini na kuvunja familia na ndoa nyingi.

“Tunajua familia nyingi ambazo zilivunjika kwa sababu baba anataka watoto waende shuleni lakini mama anakataa kwa sababu ni mfuasi wa kanisa hilo. Kuna familia nyingine ambapo wamama walitoroka na watoto na hadi wa leo hawajulikani waliko,” akasema.

Alionya wakazi dhidi ya kujipata katika mitego aina hiyo kwani inadaiwa kuna visa ambavyo waombezi huwanajisi watoto wanapoplekewa kuombewa wakidai kuwa wanawaponya.

Alitoa mfano wa kisa cha wasichana 13 kutoka kijiji cha Kinarani eneo bunge la Kaloleni, walionajisiwa na mhubiri na baadhi yao kuwa wajawazito kati ya mwaka wa 2019 na 2020.

Mwenyekiti wa Baraza la Wahubiri na Maimamu katika eneo la Pwani, Askofu Amos Lewa wa kanisa la Joy Fellowship, alikiri kuwepo kwa tabia hiyo inayoendelezwa na baadhi ya watu ambao hawana makanisa halali.

Alioa wito kwa vyombo vya usalama kuwakama ta kuwachukulia hatua za kisheria wahubiri hao.

  • Tags

You can share this post!

Nitajitenga na Mudavadi iwapo ataungana na Ruto, Nyaribo...

Mbunge aahidi mabadiliko akilenga ugavana Mombasa

T L