• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Je tutajifunza lini?

Je tutajifunza lini?

HATUA ya Wakenya kutojifunza kutokana na mikasa iliyopita ambapo mamia ya watu waliangamia wakichota petroli baada ya matrela ya mafuta kuanguka, imesababisha tena vifo vya watu 13.

Watu wengine 31 walijeruhiwa vibaya kwenye mkasa uliotokea Jumamosi jioni, katika eneo la Malanga, Kaunti ya Siaya.Kulingana na Mkuu wa Polisi wa Gem Moreso Chacha, trela hiyo iligongana moja kwa moja na lori lililokuwa limebeba maziwa katika Barabara ya Kisumu kuelekea Busia.

Lori la Maziwa lilikuwa likitoka Busia kuelekea jijini Kisumu.Licha ya kuwepo kwa marufuku ya kuzuia watu kutoka nje kuanzia saa moja jioni kwa lengo la kuzuia maambukizi ya virusi vya corona, wakazi wa eneo hilo waliikiuka na kukimbia kuchota mafuta saa tatu usiku.

Trela hiyo ililipuka sekunde kadhaa baada ya mmoja wa wakazi kufungua kifuniko ili mafuta yamwagike waanze kuchota.Bw Chacha alisema kuwa maafisa wa polisi walipata tayari gari hilo la mafuta limelipuka.

Kulingana na Bw Paul Manasseh, mmoja wa wahudumu wa bodaboda waliosaidia kukimbiza majeruhi katika hospitali mbalimbali, kati ya waliofika katika eneo la tukio kuchota mafuta, alikuwa mwanamke mjamzito na mwingine aliyekuwa amebeba mtoto mgongoni.

Bw Manasseh alisema waliwasaidia manusura kwa kuzima moto wakitumia matawi ya miti na kuwamwagia mchanga kabla ya kuwakimbiza hospitalini.Baadhi ya wagonjwa waliolemewa sana walipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Siaya.

“Mwanamke mjamzito na mwingine aliyekuwa amebeba mtoto mgongoni waliangamia kwenye moto huo. Hali ilikuwa mbaya sana katika eneo la mkasa,” akasema Bw Manasseh.Miili ya walioangamia ilitolewa katika eneo la mkasa kwa kutumia wilibaro.

Mmoja wa wapita njia aliyetambuliwa kwa jina la Oloo alijeruhiwa vibaya baada ya nguo zake kushika moto kabla ya kusaidiwa na wahudumu wa bodaboda.Jana asubuhi, mifupa ya watu walioteketea kiasi cha kutotambuliwa ilitapakaa kila mahali katika eneo hilo.

Aidha, kulikuwa na pikipiki iliyoteketea – kumaanisha kuwa huenda mmoja wa walioteketea alikimbia kuchota mafuta kwa kutumia pikipiki.Familia za waathiriwa ziliangua kilio huku nyingine zikizunguka hospitalini kutafuta wapendwa wao.

Mkasa huo ulitokea umbali wa kilomita nne kutoka eneo la Sidindi ambapo mkasa sawa na huo ulitokea mnamo Julai 1998 na kusababisha vifo vya watu 39 walioteketea wakichota mafuta.Bw Chacha alisema huenda idadi ya majeruhi iko juu kwa kuwa huenda baadhi yao walitoroka wakihofia kukamatwa na polisi.

Alisema polisi kwa kushirikiana na maafisa wa zimamoto kutoka Kaunti ya Busia baadaye waliuzima moto huo.“Hatukupata gari la zimamoto katika Kaunti ya Siaya kwani limepelekwa jijini Nairobi ambapo linafanyiwa ukarabati,” akasema Bw Chacha.

Mnamo 2009, watu 77 waliungua na kusalia majivu baada ya kuteketea wakichota petroli, gari la mafuta lilipoanguka katika eneo la Sachangwan katika barabara ya Nakuru- Eldoret.Waathiriwa walizikwa katika kaburi la pamoja katika eneo la mkasa huo.

Mbunge wa Gem, Elisha Odhiambo alishutumu Mamlaka ya Barabara Kuu nchini (KeNHA) kwa kutoweka bango la kuonyesha kuwa eneo hilo ni hatari. ‘Mamlaka ya KeNHA inafaa kuwajibika. Eneo hili limekumbwa na visa vingi vya ajali lakini hakuna bango la kuonyesha kwamba ni hatari,” akasema Bw Odhiambo.

  • Tags

You can share this post!

Miaka 10 baada ya ugonjwa wa Rinderpest kuondolewa duniani,...

Dadake Raila adai tenda zatolewa kwa upendeleo