• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
Dadake Raila adai tenda zatolewa kwa upendeleo

Dadake Raila adai tenda zatolewa kwa upendeleo

DADAKE kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, amekashifu vikali Halmashauri ya Usimamizi wa Bandari nchini (KPA) kwa madai ya mapendeleo kwenye taratibu za utoaji zabuni za bandari mpya ya Kisumu.

Bi Ruth Odinga alisema japo wenyeji wa eneo la Magharibi wamefurahia mno mradi huo pamoja na mingine katika ukanda huo, alisisitiza kuwa wanakandarasi pamoja na jamii za kutoka eneo hilo ndizo zinafaa kufaidika na ujenzi huo.

Bi Odinga alihudumu kama Naibu Gavana wa Kaunti ya Kisumu kati ya 2013 na 2017.Alieleza kusikitishwa na hatua ya kandarasi nyingi kupewa kampuni za kutoka Nairobi na Pwani, hali inayowanyima nafasi wawekezaji kutoka eneo hilo kufaidika kutokana na mradi huo.

Alisema lazima halmashauri hiyo, Halmashauri ya Huduma za Reli (KR) na Mamlaka ya Kusimamia Shughuli za Majini (KMA) kufanya utathmini mpya ili kuhakikisha wawekezaji katika eneo hilo wamefaidika kutokana na miradi mikubwa ya maendeleo inayoendeshwa na serikali ya kitaifa.

“Namshukuru Rais Uhuru Kenyatta na nduguye Raila Odinga kwa kuanzisha miradi inayoendelea jijini Kisumu na eneo la Magharibi. Hata hivyo, lazima pawe na juhudi kuhakikisha wenyeji wamefaidika kutokana nayo,” akasema kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Alisema lazima KPA ijaribu kuhakikisha kuna usawa katika utoaji wa kandarasi kwa kampuni mbalimbali, hasa inapojitayarisha kuanza harakati za kukarabati barabara katika maeneo ya Luanda Kotieno, Kendu Bay na Muhuru Bay.

“Hatuzungumzii kandarasi ndogo pekee, lakini hata kandarasi zile kubwa. Baadhi ya kampuni zilizokuwa zikitafuta nafasi ya kupewa kandarasi hizo zilinyimwa ilhali zina uwezo wa kuzitekeleza,” akasema.

Alisema miji mikubwa kama Kisumu ilikua na kustawi kiuchumi kutokana na uwepo wa reli. Hivyo, alieleza lazima masoko yaliyo karibu na reli inayoelekea katika eneo hilo yaboreshwe.“Ni lazima mashirika hayo ya serikali yazisaidie jamii kwa kujenga miundomsingi kama shule na kuboresha masoko mbalimbali ili kuhakikisha zinafaidika kutokana na miradi hiyo,” akasema.

Aliongeza kuwa si haki kwa mashirika hayo kuendelea kubomoa biashara za wenyeji ilhali ndizo wanategemea kujikimu kimaisha, ikiwa hawatafaidika kutokana na miradi inayoendelea kutekelezwa. “Ni kutokana na hayo ambapo nitaendelea kusisitiza kuhusu haja ya watu wetu kuona faida za miradi hii,” akasema.

Hata hivyo, Meneja Mkuu wa Ustawishaji Miundomsingi katika halmashauri , Bw Vincent Sidai alisema kuwa shughuli zote zinazoendelea katika bandari hiyo zinaendeshwa humo. Alisema ni idara inayosimamia utoaji kandarasi pekeeinayoweza kujibu maswali yanayohusiana na taratibu zinazozingatiwa.“Hayo ni masuala yanayosimamiwa na Meneja Mkuu wa Mahusiano ya Kibiashara,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Je tutajifunza lini?

Wandani wa Ruto wamtaka kinara wa ODM astaafu siasa