• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 AM
‘Jicho Pevu’ ashambulia familia ya Gavana Joho

‘Jicho Pevu’ ashambulia familia ya Gavana Joho

Na WINNIE ATIENO

MBUNGE wa Nyali, Bw Mohamed Ali amemkashifu Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho na jamaa zake akidai wanahujumu mipango yake ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika eneo bunge lake.

Bw Ali ambaye ni maarufu kama ‘Jicho Pevu’ alisema Bw Joho anatumia mbinu hizo kwa kuwa ameisha kisiasa.

Katika mahojiano maalumu na Taifa Leo, mbunge huyo alidai kuwa Bw Joho, nduguye ambaye ni bwanyenye maarufu, Abu Joho na jamaa yao Said Abdalla wanampiga vita ambavyo vinaathiri wananchi wanaonyimwa maendeleo hata kutoka kwa serikali ya kaunti.

“Bw Joho awaelezee Wakenya mradi wowote ambao aliuanzisha eneo la Nyali. Eneo langu limetengwa na kubaguliwa kwa sababu za kisiasa. Lakini Bw Joho anasahau kuwa anawaadhibu walipa ushuru wala si Mbunge wao. Unawaumiza wakazi waliompigia kura,” akasema.

Mbunge huyo ambaye ni mwandani wa Naibu Rais William Ruto, alidai masaibu hayo yanatekelezwa kwa ushirikiano na serikali kuu, kupitia kwa mshirikishi wa eneo hilo, Bw John Elungata.

Juhudi zetu kutafuta maoni kutoka kwa Gavana Joho na kaka yake hazikufua dafu, lakini Bw Abdalla alipuuzilia mbali madai ya Bw Ali.

“Sijawahi kuingilia miradi yake. Kwa mfano, suala la Freretown, uwanja huo ni wa kijamii kwa hivyo uko chini ya Serikali ya Kaunti ya Mombasa. Gavana anapanga kujenga uwanja wa michezo,” akasema, huku akimwambia Bw Ali aache kueneza uongo.

Kwa upande wake, Bw Elungata alikataa kujadili suala hilo na kuambia Taifa Leo kuwa, Bw Ali ndiye anayefahamu kile anachozungumzia.

Bw Ali alisema alipata Sh21 milioni kujenga shule ya sekondari la Ziwa la Ngombe, lakini mwanakandarasi alipigwa na kufukuzwa na vifaa vyake vya kazi kuharibiwa.

Katika eneo la Mwatamba, mbunge huyo alisema alipanga kujenga afisi ya chifu na naibu kamishna wa kaunti lakini alizuiliwa na serikali ya kaunti.“Kwa hivyo miradi inayogharimu Sh40 milioni imesimamishwa,” akasema.

Kuhusu madai kwamba maisha yake yamo hatarini, mbunge huyo alisema hawezi kupiga ripoti kwa polisi kwa sababu awali aliwahi kufanya hivyo lakini hakuna hatua iliyochukuliwa kumlinda.

Alisema alipiga ripoti kwa polisi dhidi ya Bw Joho pia wakati wa uchaguzi mdogo wa Msambweni lakini hakuchukuliwa hatua. “Niwashtaki wapi sasa?” akauliza.

You can share this post!

Itikadi na miko ya Uswahilini ambayo haihusiani na dini

Ogiek, Ndorobo waomba kikao na Rais kuhusu ardhi