• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
JSC yateua Martha Koome kuwa Jaji Mkuu

JSC yateua Martha Koome kuwa Jaji Mkuu

Na RICHARD MUNGUTI

JAJI Martha Koome anakaribia kuandikisha historia kuwa Jaji Mkuu wa kwanza mwanamke nchini, baada ya Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kupendekeza jina lake Jumanne.

Sasa macho yote yako bungeni kuona kama litamwidhinisha au la. Tangazo la uteuzi wa Jaji Koome lilifuatia kufutiliwa mbali kwa agizo la kusimamisha mchakato wa kumsaka mrithi wa Bw David Maraga na rais wa mahakama ya rufaa.

“JSC imeandikisha historia kwa kumteua mwanamke wa kwanza kuwa Jaji Mkuu wa Kenya,” mwenyekiti wa jopo la zoezi hilo Prof Olive Mugenda.

Katika taarifa kwa wanahabari Prof Mugenda alisema, “baada ya kutafakari na kujadialiana kwa kina kuhusu kila mwaniaji, JSC imempendekeza Jaji Martha Koome Karambu wa Mahakama ya Rufaa kuwa Jaji Mkuu mteule.”

Prof Mugenda alisema jina la Jaji Koome litapelekwa kwa Rais Uhuru Kenyatta kumteua. Bunge litepelekewa jina la Jaji Koome na kamati ya bunge itamhoji kisha kujadiliwa na bunge kabla ya kuidhinishwa.

JSC iliwapongeza wananchi na wote walioshiriki katika mchakato huo wa uteuzi wa Jaji Mkuu wa 15 tangu Kenya ijinyakulie uhuru.

Prof Mugenda hakufichua kura alizopata Jaji Koome ndipo awabwange wawaniaji wengine tisa walioomba kiti hicho.

Wengine waliowania wadhifa huo wakili redrick Ngatia, rais wa mahakama ya rufaa Jaji William Ouko , Majaji Said Juma Chitembwe, Mathew Nduma Nderi, David Marete, wasomi Prof Kameri Mbote Annie Patricia Gathiru, wakili Philip Murgor, Prof Dkt Dkt Moni Wekesa na wakili Alice Yano.

Jaji Koome aliyezaliwa katika kaunti ya Meru 1960 aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu 2003 na Jaji wa Mahakama ya rufaa 2012.

Kabla ya kuteuliwa Jaji alikuwa akishiriki katika kesi nyingi za kutetea haki za binadamu akiwa mwanachama wa chama cha mawakili wanawake –Fida.

Alikuwa katika msitari wa mbele kupinga serikali ya Kanu chini ya uongozi wa hayati Daniel arap Moi. Jaji Koome mwenye umri wa miaka 61 alikuwa ametayarisha manifesto ya kuboresha utendakazi katika idara

Sasa Mahakama ya Juu itakuwa na rais mwanamke. Naibu wake atakuwa Jaji Philomena Mwilu. Sasa Mahakama ya Juu itakuwa na wanawake watatu Jaji MkuuKoome, Jaji Mwilu na Jaji Njoki Ndung’u.

Jaji Koome atakuwa na kibarua kigumu kuamua kesi ya kupinga uchaguzi wa urais 2022 iwapo itawasilishwa. Jaji Koome aliokoa nchi 2017 alipotoa uamuzi usiku wa kuruhusu uchaguzi wa rais uendelee 2017.

Mahakama kuu ilikuwa imeupiga kalamu uchaguzi huo wa pili wa urais ikisema tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) haikuwa imewateua maafisa wa usimamizi kulingana na sheria.

Jaji Koome aliitwa kutoka mahakama ya Malindi kusikiza na kuamua kesi hiyo. Prof Mugenda alitangaza zoezi la kumteua Jaji wa Mahakama ya Juu kutwaa nafasi ya Jaji Jackton Ojwang aliyestaafu itaendelea Mei 3,2021.

Awali Majaji Roselyn Nambuye, Sankale ole Kantai na Patrick Kiage walifutilia mbali agizo la kuisitisha zoezi la kumsaka mrithi wa Bw Maraga.

Majaji hao walisema hafla ya kumsaka Jaji Mkuu mpya ni zoezi lenye umuhimu mkubwa kwa nchi hii.

You can share this post!

TANZIA: Mhariri wa zamani wa Taifa Leo afariki

FAUSTINE NGILA: Tuwazime wafisadi iwapo tunataka teknolojia...