• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Kaunti kutumia zaidi ya 42m safari za nje

Kaunti kutumia zaidi ya 42m safari za nje

Na DERICK LUVEGA

SERIKALI ya Kaunti ya Vihiga inapendekeza kuongeza mara tatu kiasi cha fedha zilizotengewa usafiri katika nchi za kigeni kwenye bajeti ya 2021/22, wakati ambapo Covid-19 imelemaza usafiri baina ya mataifa.

Usimamizi wa kaunti hiyo unapendekeza kumimina kitita kingine cha Sh12.6 milioni kwa shughuli hiyo kuanzia Julai 1, kutoka Sh3.1 milioni ambazo tayari zimetumika katika bajeti hiyo hiyo ya, 2020/21.

Matumizi hayo ya fedha yaliyopendekezwa yamo katika bajeti ya 2021/22 ambayo inakaguliwa na umma.

Kiasi cha Sh12.6 milioni ni sehemu ya Sh54.7 milioni zitakazotumika katika shughuli za usafiri nchini na katika mataifa ya kigeni katika bajeti mpya iliyoongezwa kutoka Sh43.2 milioni, zilizotumika kwa ziara hizo mwaka huu.

Hii inaashiria kuwa uongozi wa Gavana Wilber Ottichilo utatumia Sh42.1 milioni kwa shughuli za usafiri nchini, iwapo mapendekezo hayo yataidhinishwa jinsi yalivyo kwa sasa.

Msimamizi Mkuu wa Bajeti katika ripoti za awali amewahi kuibua maswali mazito kuhusu matumizi hayo ya fedha kwenye ziara za kigeni na humu nchini.

Akizungumza katika kikao cha kushirikisha umma hivi majuzi kuhusu bajeti hiyo ya Sh5.8 bilioni, Waziri wa Fedha Alfred Indeche alikiri kuwa janga la virusi vya corona limetatiza shughuli.

Alisema kutokana na hali hiyo, kaunti inatilia maanani tu miradi inayoendelea huku kukiwa na upunguzaji wa bajeti pamoja na deni la zaidi ya Sh1 bilioni za ada ambazo hazijalipwa.

Serikali ya kaunti inakabiliwa na uhaba wa Sh700 milioni huku Bw Indeche akihimiza wafanyabiashara kusaidia serikali ya kaunti hiyo kukusanya kiasi cha Sh192.7 milioni kutoka kwa mapato yao binafsi.

Katika bajeti iliyopendekezwa, idara ya ardhi itatumia kiasi kikuba zaidi cha fedha katika ziara za kigeni cha Sh3 milioni.

Inafuatiwa na afisi ya gavana na idara za afya na maji ambazo zitatumia Sh2 milioni kila moja kwa ziara za kigeni.

Idara za fedha na umma zimetengewa kiasi kilichopendekezwa cha Sh1 milioni kila moja, zitakazotumika kwa ziara za kigeni.

Idara za kilimo na biashara ndizo zitakazotumia kiasi cha chini zaidi katika ziara za kigeni baada ya kutengewa kila mmoja kiasi kilichopendekezwa cha Sh800,000.

Idara za elimu, michezo, bodi ya kaunti kuhusu huduma za umma, usafiri na miundo msingi, hazijatengewa fedha za usafiri katika mataifa ya kigeni.

Hata hivyo, kulingana na makadirio hayo, idara ya fedha, itatumia kiasi cha hadi Sh12.8 milioni katika ziara za humu nchini ikifuatiwa na idara ya afya kwa Sh9 milioni.

Ziara za humu nchini zitaigharimu afisi ya gavana Sh3.7 milioni, kiasi sawa na idara ya huduma ya umma, idara ya usafiri na miundomsingi (Sh3.4milioni) na kilimo (Sh2.5 milioni).

Katika mapendekezo hayo, idara ya ardhi imetengewa Sh3 milioni na kiasi kingine cha Sh1 milioni kwa kila moja wa idara zake.

  • Tags

You can share this post!

NASAHA ZA RAMADHAN: Tujibidiishe kuamka kumi hili la mwisho...

TAHARIRI: Ziara ya Suluhu ifufue uhusiano