• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
NASAHA ZA RAMADHAN: Tujibidiishe kuamka kumi hili la mwisho lenye usiku wa Laiyatul Qadir

NASAHA ZA RAMADHAN: Tujibidiishe kuamka kumi hili la mwisho lenye usiku wa Laiyatul Qadir

Na SHEIKH MOHAMMED KHALIFA

MSOMAJI mpendwa tunakutana tena ndani ya mwezi wa Ramadhani.

Hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu (SWT) kutufikisha Ramadhani nyingine.

Alhamisi ya leo ninaanza na swali la ndugu yetu Abubakar Khamis kutoka Majengo Vihiga anayeuliza, “Mwanzoni mwa Ramadhani tulianza kufunga tukiwa makundi mawili. Je, tutajuaje ni ipi siku sahihi ya Lailatul Qadir?”

Bismillhi Rahamani Rahim. Kwanza kwa wasomaji wasioelewa anachouliza ndugu Abubakar ni kwamba, Lailatul Qadir ni usiku wenye hadhi kubwa katika siku 10 za mwisho za Ramadhani. Tuko katika siku hizo 10 za mwisho.

Bwana Mtume Muhammad (SAW) aliwahi kueleza kwamba awali alikuwa akiijua siku halisi inayokuwa usiku wa cheo.

Lakini Mwenyezi Mungu (SWT) akamsahaulisha. Alichokumbuka ni kuwa siku hiyo, ambayo Waislamu wanaamini ubora wake ni sawa na miezi 1,000 au miaka 83, umo kwenye siku za witri (zisizogawika kwa mbili). Yaani siku za 21, 23, 25, 27 au 29.

Sasa hapa ndipo ambapo ndugu Abubakar anauliza, kwa vile kuna watu waliotangulia kufunga Aprili 13 na wengine wakafunga Aprili 14, kuna wanaohesabu kuwa leo ni siku ya 24 na wenzao wako siku ya 23. Kwa hivyo watajua vipi siku inayostahili kuwa ya kutarajia huo usiku wa Laylatul Qadir?

Kwanza Laylatul Qadir ni siri yake Mwenyezi Mungu (SWT). Hakuna mtu yeyote anayeijua. Ni Mapenzi yake yeye Mwenyezi Mungu kumfanya Mtume Muhammad (SAW) asiweze kuitaja ni siku gani.

Kwan hivyo hii haina mtu wa kwanza wala wa mwisho. Kwanza ukiangalia masuala ya Fiqhi (elimu ya sheria katika Uislamu), wasomi karibu wote wa Kiislamu kama akina Ibn Taimiya, Al Bani, Ibn Baazi na wengineo wanakubali kwamba ni sawa watu kufunga kwa mwezi mmoja (yaani mwezi ukionekana eneo moja ulimwengu mzima ufuate) na ni sawa watu kufunga kwa mwezi ule wa nchi yao watakapouona.

Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu rehema zake zimeenea kila mahali. Kilicho muhimu ni mja kujishughulisha zaidi katika ibada katika siku hizi zilizobaki, akiwa na matarajio kuwa Mwenyezi Mungu (SWT) ataziona juhudi zake.

Mtu ataandikiwa yatakayolingana na juhudi zake katika kujitolea kufanya ibada, bila ya kujali kama ni yeye aliyeanza kufunga au mwenzake aliyechelewa siku moja, atakayeipata siku hiyo ya Laiyatul Qadir.

Iwapo utabaki kwenye ibada usiku katika siku 10 za mwisho, au kuanzia usiku wa leo hadi mwisho wa Ramadhani, bila shaka utakuwa umeupata usiku huo wenye fadhila hizo kubwa.

You can share this post!

Mashabiki wa Real Madrid wataka usimamizi wa klabu hiyo...

Kaunti kutumia zaidi ya 42m safari za nje