• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Kaunti yachukua hatua kudhibiti homa ya dengue

Kaunti yachukua hatua kudhibiti homa ya dengue

Na WACHIRA MWANGI

MAAFISA wa afya ya umma Kaunti ya Mombasa, wameweka mikakati ya kufuatilia na kuzuia kusambaa kwa homa ya dengue.

Haya yanajiri siku chache baada ya maafisa wa afya ya umma kuonya kuwa, kuna mkurupuko wa homa hiyo katika kaunti hiyo.

Kulingana na Afisa Mkuu wa Afya ya Umma Bi Pauline Oginga, ugonjwa huo umekuwa ukiongezeka tangu Februari mwaka huu na sasa ameonya umma kuwa waangalifu kuuzuia.

Aliwataka wakazi kutaocha matangi ya maji yakiwa wazi ili kupunguza maeneo ya mbu kuzaana.

Serikali ya kaunti inashirikiana na vijana wa Kazi Mtaani kuzibua mitaro ya maji taka.

Bi Oginga alieleza kwamba wanatumia wafanyakazi wa afya wa kujitolea kuhamasisha umma kuhusu maradhi na jinsi wakazi wanaweza kuzuia kusambaa kwake.

Takwimu za kila wiki kutoka kwa maafisa wa kufuatilia magonjwa katika kaunti ya Mombasa zinaonyesha kuwa, kuanzia Januari 2021, watu wazima na watoto wasiokuwa na dalili za malaria walipatikana kuwa na homa ya dengue.

Miezi miwili iliyopita imetajwa kuwa ya mkurupuko wa ugonjwa huo huku wagonjwa wakionyesha dalili hatari.

“Mgonjwa anaweza kuwa katika hali mbaya na kulazwa hospitali akiwa na dalili mbaya za ugonjwa huo kwa kuwa unaathiri viungo muhimu vya mwili. Mtu anaweza kutokwa damu; hivi ndivyo homa ya dengue ilivyo hatari,” alionya Bw Oginga.

Alisema kwamba sampuli za damu zilitolewa kutoka kwa wagonjwa walioshukiwa kuwa na homa hiyo katika kaunti hiyo kati ya Machi na Aprili na kufichua kwamba watu 24 kati ya kila 47 ikiwa ni asilimia 51 walikuwa na homa ya dengue.

Changamwe na Jomvu zilikuwa na watu saba waliokuwa na homa hiyo,Kisauni 6, Nyali 4 na Likoni 2. Hakukuwa na na sampuli kutoka eneobunge la Mvita.

Bi Oginga alisema kwamba, wengi wa wagonjwa hawakuwa na dalili za ugonjwa huo kumaanisha wanaambukizwa lakini hawapati dalili na kwamba wachache walizidiwa na maradhi hayo.

Dalili za ugonjwa huwa ni kuumwa na kichwa, joto, kutapika, maumivu ya tumbo na kuumwa na misuli.

Maafisa wa afya ya umma wanasema ni vigumu kutofautisha homa ya dengue na malaria na wanahimiza wote wanaohisi dalili hizi kutafuta matibabu hospitalini.

  • Tags

You can share this post!

Mahanga adhihirisha uaminifu wa dhati kwa Obado

Waliokaa jela miaka 22 hatimaye huru