• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Kawira alijipandisha mwenyewe kwenye karandinga, Polisi wajitetea

Kawira alijipandisha mwenyewe kwenye karandinga, Polisi wajitetea

NA LABAAN SHABAAN

IDARA ya Kitaifa ya Huduma ya Polisi (NPS) imejitetea kuhusu taarifa ya kukamatwa kwa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza.

Gavana huyo alionekana kwenye karandinga ya polisi Jumatano, Oktoba 18, 2023.

Inspekta Jenerali wa Polisi Japheth Koome alikana kuwa polisi walimkamata Bi Mwangaza aliyekuwa anaendeleza hafla zake za msaada kwa jamii eneo la Imenti ya Kati.

Mnamo Jumatano, gavana huyo alidai alishikwa na polisi alipokuwa akitoa msaada wa ng’ombe kwa familia katika mpango wake wa Okolea Outreach.

Baadaye Bi Mwangaza alisema ameachiliwa bila masharti na Mkuu wa Kituo cha Polisi (OCS) cha Ruiga ya Kati.

Gavana Mwangaza alidai OCS alimwomba msamaha kwa kumzuilia kinyume cha sheria ndani ya gari la polisi.

“Hatimaye. Niko Huru. Namshukuru Mungu niko salama. OCS ameomba msamaha,” alisema.

Kulingana na bosi wa polisi, gavana huyo alipanga sarakasi kwa sababu alizojua mwenyewe.

Bw Koome alisema Bi Mwangaza alijipandisha kwenye gari la polisi kimakusudi na pia kushuka polisi wakimwangalia huku kamera zikimnasa.

“Gavana alipanda gari la polisi kwa kupenda na kushuka baadaye. Kwa kweli, taarifa ya Bi Kawira kwa vyombo vya habari haitaji kuwa polisi walimtia mbaroni. Ila alitaja kuwa kulikuwa na polisi wengi mkutanoni mwake,” Bw Koome alisema katika taarifa yake ya Oktoba 19, 2023.

Kauli ya Mkuu wa Polisi ilijiri baada ya Baraza la Magavana (CoG) kukashifu tukio la ‘kukamatwa’ kwa gavana mwenzao.

Magavana walitaka Bw Koome kuomba Bi Mwangaza msamaha mbele ya umma kuhusiana na suala hilo.

“Magavana wanataka polisi wamwombe Bi Mwangaza msamaha hadharani kwa kumuaibisha, usumbufu, udhalilishaji na kumdhihaki mbele ya umma,” sehemu ya taarifa ya magavana ilisema wakiteta polisi wamezoea kuwatisha.

Gavana huyu wa mara ya kwanza anakabiliwa na shinikizo kutoka kwa wajumbe wa Kaunti ya Meru wanaoendeleza hoja ya kumbandua mamlakani kwa mara ya pili baada ya jaribio la kwanza kufeli.

Hoja hiyo iliwasilishwa bungeni Meru na Kiongozi wa Wengi Evans Mawira Oktoba 17, 2023.

Bi Mwangaza anatuhumiwa kwa mapendeleo na utumizi mbaya wa rasilimali miongoni mwa shutuma nyingine.

  • Tags

You can share this post!

KCB RFC yavizia Menengai Oilers katika nusu-fainali ya...

Wanamapinduzi Niger wadai wamezima jaribio la Rais Bazoum...

T L