• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 7:02 PM
Kenya yavuma kwa ulanguzi wa pesa

Kenya yavuma kwa ulanguzi wa pesa

Na MARY WAMBUI

KENYA imetajwa katika bunge la Amerika kuwa miongoni mwa nchi zinazotumiwa kwa ulanguzi wa pesa zinazotumika kufadhili ugaidi na maovu mengine kimataifa.

Kulingana na ripoti iliyowasilishwa katika bunge hilo, hali hii imechangiwa na ongezeko la matumizi ya kutuma pesa kwa njia ya simu, mfumo wa benki wa hawala na kutakasa pesa zilizopatikana kwa njia ulanguzi kupitia biashara.

Kenya imeorodheshwa miongoni mwa nchi hatari kwa ulanguzi wa pesa kote ulimwenguni huku zaidi ya Sh17.8 bilioni zikitumwa kutoka nchi za nje kati ya Januari na Agosti 2020.

Baadhi ya pesa hizi zinashukiwa kupatikana kupitia biashara ya dawa za kulevya.

Nchi nyingine zilizotajwa katika orodha hiyo ni Nigeria, Ghana, Liberia, Morocco, Msumbiji, Tanzania, Algeria na Benin.

Nchi za ng’ambo zilizotajwa kwenye orodha hiyo ni Cyprus, Cuba, Italia, Mexico, Uturuki, Milki ya Uarabu, Vietnam, India, Visiwa vya Cayman, Amerika, Uingereza na Colombia miongoni mwa nyingine.

Ripoti hiyo iliyochapishwa na serikali ya Amerika inasema licha ya athari za janga la corona kwa uchumi wa mataifa mengi ulimwenguni, pesa haramu ziliendelea kumiminika.

“Wahalifu hawakuendeleza uhalifu wa kawaida wa kifedha, mbali pia walibuni njia mpya za kutumia janga hilo kwa kuunda bidhaa feki, simu na barua pepe bandia kutangaza bidhaa za afya au matibabu,” inasema ripoti hiyo.

Inasema hali hii ilitokana na ufisadi katika maeneo mengi uulimwenguni.

Ikiwa na uchumi mkubwa Afrika Mashariki na ya kwanza kubuni mfumo wa kutuma pesa kwa simu, Kenya inakabiliwa na hatari ya kutumiwa na walanguzi wa pesa na ufadhili wa ugaidi kupitia uhalifu wa mitandao, ufisadi, ulanguzi wa bidhaa za wanyama, ulanguzi wa dawa za kulevya na biashara haramu ya mbao na makaa.

Ikiwa kituo muhimu cha kupitia eneo hili na kuwa jirani wa Somalia, Kenya ni kivutio kwa ulanguzi wa pesa zinazopatikana kutokana na uharamia, biashara isiyothibitiwa ya miraa na makaa.

You can share this post!

Mtihani wa gredi ya nne wakumbwa na matatizo maeneo mengi...

Kaunti zaanza kupeana chanjo