• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Kesi za ufisadi: Haji ajitetea

Kesi za ufisadi: Haji ajitetea

Na CHARLES WASONGA

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DDP) Noordin Haji ametetea afisi yake dhidi ya shutuma kutoka kwa baadhi ya wanasiasa kwamba haiendeshi kazi zake kwa njia huru inaposhughulikia kesi za ufisadi.

Kwenye mahojiano katika Runinga na NTV Jumanne jioni Bw Haji alifafanua kuwa afisi yake hutegemea ushahidi unaowasilishwa na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kabla ya kuamua ikiwa kesi inafaa kuwasilishwa kortini au la.

“Afisi yangu huwa haifanyi uchunguzi wa kesi za ufisadi. Sisi hutegemea matokeo kutokana na uchunguzi wa DCI haswa kuhusu kesi zote za aina hii, zikiwemo zinazowahusu wanasiasa,” akaeleza kwenye mahojiano na mwanahabari Lofty Matambo.

Akaongeza: “Tumewahi kulaumiwa na watu wengi. Binafsi, nimeelekezewa shutuma nyingi. Tunaposhughulikia kesi kuhusu mwanasiasa kutoka mrengo fulani, mimi hushutumiwa na wanasiasa kutoka mrengo huo. Lakini kazi yetu huwa ni kupokea faili ya uchunguzi na kuikagua kwa kina ili kubaini ikiwa kuna ushahidi tosha wa kuruhusu kufunguliwa kwa mashtaka.”

Kuhusu kesi ya ufisadi inayomkabiliwa Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua, DPP alisema kuwa afisi yake imepokea ushahidi wa kutosha kutoka DCI wa kuweza kuhimili mashtaka.

“Tumepokea faili ya uchunguzi yenye ushahidi wa kutosha kwamba Bw Gachagua alipora fedha za Hazina ya Ustawi katika eneobunge lake kando na kujihusisha katika ulanguzi wa fedha,” Bw Haji akasema.

DDP alieleza kuwa ni kwa msingi wa ushahidi huo kutoka kwa afisi ya mkurugenzi wa DCI George Kinoti ndipo kesi hiyo iliweza kufikishwa mahakamani.

Bw Haji alisema maafisa wake wako tayari kuthibitisha mbele ya mahakama kwamba Bw Gachagua alishiriki ufisadi na wizi wa pesa za umma.

Alisema hayo saa chache baada ya Bw Gachagua kuachiliwa huru na mahakama moja ya Nairobi kwa kupewa dhamana ya Sh12 milioni na mdhamini wa kiasi sawa na hicho.

Mbunge huyo alikuwa amefikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Lawrence Mugambi akibilisha na mashtaka ya kupokea Sh12 bilioni kwa njia ya ufisadi.

Hata hivyo, stakabadhi za mashtaka zilionyesha kuwa Bw Gachagua alishtakiwa kwa kosa la kupokea Sh7.4 bilioni kinyume cha sheria na ulanguzi wa fedha.

Hata hivyo, mbunge huyo alikana madai hayo, kwamba alipokea fedha hizo kupitia zabuni ambazo kampuni zake zilipata katika serikali ya Kaunti ya Nyeri na ile ya Kitaifa, kinyume cha sheria.

Inadaiwa kuwa mwanasiasa huyo alitenda makosa hayo kati ya miaka ya 2013 na 2020. Alishtakiwa pamoja na wengine ambao hawakuwa kortini.

Bw Gachagua ambaye alikamatwa mnamo Ijumaa wiki jana, nyumbani kwake Sagana, Nyeri, alidai kuwa hatua hiyo ilichochewa kisiasa kutokana na mchango wake katika kushindwa kwa chama cha Jubilee katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Kiambu.

Wanasiasa wa mrengo wa Tangatanga wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto pia walitoa madai sawa na hayo wakiisuta serikali kwa kupanga njama ya kuwakamata wanasiasa mrengo huo na kuwasingizia mashtaka.

“Pole sana ndugu yangu Bw Gachagua. Nafahamu wazi kwamba umekamatwa kutokana na sababu za kisiasa na kwamba sababu wewe ni rafiki yangu,” Dkt Ruto akasema kupitia Twitter.

You can share this post!

Mshtuko wezi wakipora benki mchana

SGR, barabara nzuri ndiyo rekodi kuu ya Uhuru –...