• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Kidero agonga mwamba

Kidero agonga mwamba

NA RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi Dkt Evans Kidero amegonga mwamba katika jitihada zake kumtimua Jaji Esther Maina katika kesi anayodaiwa alijitajirisha na Sh68 milioni pesa za umma.

Serikali inaomba Mahakama Kuu iamuru Dkt Kidero anyang’anywe pesa hizo.

Jaji Maina alikataa kujiondoa katika kesi hiyo akisema akijing’atua ataweka historia mbaya katika idara ya mahakama kwa vile washukiwa watakuwa na mazoea mabaya ya kumtimua hakimu au jaji katika kesi wanapojihisi mambo yanawaendea mrama.

Alisema ombi hilo la Dkt Kidero halina mashiko kisheria na kulitupilia mbali.

Katika kesi hiyo Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadii (EACC) inaomba mahakama iamuru Dkt Kidero anyang’anywe Sh68 milioni mali ya umma anayodaiwa alipokea kwa njia isiyo halali.

Dkt Kidero aliyewania kiti cha Ugavana cha Homa Bay uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 na kushindwa na Bi Gladys Wanga aliomba Jaji Maina ajiondoe katika kesi hiyo ya EACC dhidi yake akidai atamwonea.

Dkt Kidero alilalama kwamba Jaji Maina hatatenda haki endapo ataendelea kusikiza kesi hiyo ya kurudishwa kwa mali ya umma aliyojinufaisha nayo.

Pia Dkt Kidero alilia kwamba Jaji Maina alikataa kusitisha kusikizwa kwa kesi inayomkabili ya ufisadi wa Sh131 milioni anayoshtakiwa pamoja na washukiwa wengine 16.

Akitoa uamuzi wake Jaji Maina alisema ombi hilo la Dkt Kidero halina mashiko kisheria na “kamwe hakuwasilisha ushahidi wowote kuthibitisha atamwonea akisikiza na kuamua kesi hiyo ya EACC.”

Jaji Maina alitupilia mbali ombi la Dkt Kidero na kuamuru iendelee hadi tamati.

Dkt Kidero ameshtakiwa kulipa Sh58 milioni kampuni ya mawakili ya Wachira Mburu & Co. Advocates mnamo Januari 7, 2014.

Wengine alioshtakiwa nao ni Wachira, Mburu, Mwangi & Company Advocates, George Wainaina Njogu, John Ndirangu Kariuki, Paul Mutunga Mutungi, Manasseh Karanja Kepha, Philomena Kavinya Nzuki, Ng’ang’a Mungai, Charity Muringo Ndiritu na Peterson Andrew Njiru.

Pia Ekaya Alumasi Ghonzour, James Mbugua, Elizabeth Wanjiru Nderitu, Alice Njeri Mundia, Hannah Muthoni Kariuki, John Ngari Wainaina na Cups Limited wamejumuishwa katika kesi hiyo.

Dkt Kidero ameeleza kwa kina jinsi kesi hiyo ilivyoimbuka mnamo Desemba 16 2010 wakati kampuni ya Kyavee Holdings Limited iliposhtaki ilyokuwa Baraza la Nairobi (NCC) katika mahakama ya kuamua kesi za biashara Milimani ikiomba ilipwe Sh3bilioni kwa kunyang’anywa tenda.

You can share this post!

Wanaharakati kortini kupinga Hazina ya Hasla, wataka...

Rais Ruto awasilisha ombi la marekebisho ya Katiba...

T L