• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Kidero akiri kutangamana na Raila aliyeambukizwa corona

Kidero akiri kutangamana na Raila aliyeambukizwa corona

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi Dkt Evans Kidero ambaye ni mmoja wa watu waliotangamana na kiongozi wa ODM Raila Odinga kabla ya kuthibitishwa kuwa na Covid-19 ametangaza kuwa atajiwasilisha hospitalini apimwe.

Dkt Kidero pia amefutilia mbali shughuli zake zote za umma wikiendi hii katika kaunti ya Homa Bay ambako amekuwa akiendesha kampeni za mapema za kiti cha ugavana.

Kwenye ujumbe katika akaunti yake ya twitter, Gavana huyo wa zamani wa Nairobi alifichua kuwa alitangamana kwa karibu na Bw Odinga katika ziara yake ya siku nne Pwani kuendesha kampeni ya kuipigia debe mswada wa BBI.

“Hamjambo Wakenya wenzangu. Namtakia Jakom (mwenyekiti) afueni ya haraka. Nilikuwa pamoja naye katika ziara ya siku nne Malindi na Mombasa wikendi iliyopita kuupigia debe mchakato wa BBI. Kufuatia ripoti kwamba anaugua Covid-19 na kwa sababu ninawajibika kwa umma, nimefutilia mbali shughuli zangu zote za wikiendi.

Nitarejea Nairobi na sasa sitahudhuria mazishi ya Askofu Elijah Kwanya katika wadi ya Karachuonyo Magharibi, Homa Bay, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 115. Naenda kupimwa corona na kufuata kanuni ya kujitenga. Kwa mara nyingine namtakia Jakom afueni ya haraka,” Dkt Kidero akasema.

Mnamo Alhamisi Bw Odinga aliwaamuru madaktari wake kutangaza kwamba amepatikana na virusi vya corona na kutangaza kuwa ataenda karantini kwa kipindi cha wiki mbili.

“Kufuatia barua yangu ya Machi 10, 2021, tumethibitisha kuwa Mheshimiwa Odinga anaugua Covid-19,” daktari wake binafsi David Olunya akasema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

“Anaendelea kupata nafuu huku akipokea matibabu na ni mchangamfu. Tunaendelea kufuatilia hali yake,” Olunya akaongeza.

Bw Odinga alisema kuwa alipatikana na Covid-19 baada ya kufanyiwa vipimo kadhaa “kwa muda wa siku mbili zilizopita.”

“Licha ya kwamba ninahisi vizuri baada ya kukaa hospitalini kwa siku chache, nimekubaliana na madaktari wangu kwamba nikae karantini ya lazima,” akaeleza.

Bw Odinga alilazwa katika Hospitali ya Nairobi Jumatatu kutokana na kile madaktari wake walisema ni uchovu baada ya kufanya kampeni kali ya siku tano eneo la Pwani kuvumisha mchakato wa BBI.

Kiongozi huyo wa ODM alikosa kuhudhuria hafla fupi iliyopangwa kufanyika katika Ikulu ya Nairobi, Jumanne Machi 9, 2021 kuadhimisha miaka mitatu baada ya handisheki kati yake na Rais Uhuru Kenyatta iliyotuliza joto la siasa nchini. Salamu hizo ya heri ilifanyika peupe mnamo Machi 9, 2018.

Bw Odinga ndiye kiongozi wa hadhi ya juu zaidi nchini kuambukizwa virusi vya corona wakati huu ambapo Kenya inashuhudia wimbi la tatu la kuenea kwa homa hiyo.

You can share this post!

Vyama vya kisiasa vitakavyohusika na fujo vitafutiliwa...

Obiri kutumia tuzo ya Forbes kama kichocheo cha kuonyesha...