• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Obiri kutumia tuzo ya Forbes kama kichocheo cha kuonyesha wenzake kivumbi mbioni Jumamosi

Obiri kutumia tuzo ya Forbes kama kichocheo cha kuonyesha wenzake kivumbi mbioni Jumamosi

Na AYUMBA AYODI

BINGWA mara mbili wa mbio za mita 5,000 duniani Hellen Obiri anapanga kusherehekea mafanikio yake ya hivi punde kwa kutwaa ubingwa wa mbio za mita 10,000 kwenye duru ya pili ya Shirikisho la Riadha Kenya (AK) uwanjani Kasarani mnamo Ijumaa.

Obiri, ambaye ni mshindi wa medali ya fedha ya mbio za mita 5,000 kwenye Olimpiki mwaka 2016, alinyakua tuzo ya michezo kwenye Tuzo za Bara Afrika za Wanawake za Forbes.

Alikuwa katika orodha ya washindi wa tuzo waliotangazwa wakati wa mkutano wa wanawake wa Bara Afrika wa wanawake wanaovuma ulioandaliwa katika Siku ya Kimataifa ya Wanawake kwa njia ya mtandao.

“Mungu amekuwa mzuri kwangu kila mara na namrudishia shukrani zangu kwa tuzo hii. Ni heshima kubwa kuwa kwenye jukwaa moja na wanawake mashuhuri kama rais wa zamani wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf,” alisema Obiri akitangaza kuwa yuko tayari kuwania taji la mbio za mita 10,000 Jumamosi.

Obiri, ambaye alihifadhi taji lake la dunia la mbio za mita 5,000 jijini Doha, Qatar mwaka 2019 alikomaliza nje ya mduara wa medali katika mbio za mita 10,000 katika nafasi ya tano, ana ari ya kuwakilisha Kenya kwenye Olimpiki katika mbio za mita 5,000 na 10,000. Michezo ya Olimpiki ni Julai 23 hadi Agosti 8 mwaka huu jijini Tokyo, Japan.

Mmoja wa wapinzani wake wakuu ni mshindi wa duru ya kwanza Daisy Cherotich aliyetawala mbio za mita 10,000 mnamo Februari 28 kwa muda wake bora wa dakika 32:19.10 ugani Nyayo.

Huku malkia wa kitaifa wa mbio za nyika Sheila Chelangat akiamua kupumzika baada ya kung’aria wapinzani katika duru ya kwanza ya mbio za mita 5,000, macho yatakuwa kwa mshindi wa mbio za mita 5,000 mwaka 2016 Sheila Chepkirui anayepigiwa upatu kutamba.

Kivumbi kinatarajiwa katika mbio za mita 100 wakati mshikilizi wa rekodi ya Kenya Mark Otieno ataonana uso kwa macho na mkimbiaji mwenye kasi ya juu msimu huu Ferdinand Omanyala. Mashindano haya yataanza na michujo leo kabla ya fainali hapo kesho.

Omanyala, ambaye alikamilisha umbali huo kwa sekunde 10.11 akisaidiwa na upepo wakati wa mbio za kupokezana vijiti na kutimka 10.19 katika wikendi ya kwanza ya mashindano haya, ametangaza kuwa anataka kukimbia chini ya sekunde 10.

“Nataka kujaribu kukimbia chini ya sekunde 10 katika siku mbili zijazo,” alisema Omanyala akiwa amejaa imani. “Nataka kupata kila kitu inavyostahili kutoka eneo la kuanzia mbio, kasi na kukamilisha.”

Lengo la Otieno ni kuandikisha muda wa kufuzu kushiriki Olimpiki wa sekunde 10.05.

“Naamini inawezekana na nataka kuijaribu sasa,” alisema Otieno, ambaye hakushiriki mkondo wa kwanza, lakini akatimka mbio za mita 200 wakati wa mashindano ya kupokezana vijiti na kuandikisha muda wa sekunde 20.86. Otieno anashikilia rekodi ya kitaifa ya mbio za mita ya sekunde 10.14 aliyoweka mwaka 2017.

Mashindano hayo yataanza saa moja na nusu asubuhi katika siku hizo mbili.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

You can share this post!

Kidero akiri kutangamana na Raila aliyeambukizwa corona

Kimanzi aibuka kocha bora wa Januari 2021 Ligi Kuu ya Kenya