• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Kikosi cha dharura chawekwa Bomet kusubiri mikasa ya El-Nino

Kikosi cha dharura chawekwa Bomet kusubiri mikasa ya El-Nino

NA LABAAN SHABAAN

KAUNTI ya Bomet haiko tayari kushuhudia marejeleo ya tukio la msururu wa mafuriko ya Chepalungu Aprili 2023.

Wakati huo, mvua kubwa iliponda makazi na kusababisha familia 700 kulala nje kwenye baridi.

Kupitia Idara ya Usimamizi wa Majanga, kaunti hiyo imeweka mpango wa dharura kusaidia kikosi cha kukabili majanga.

Kikosi hiki kimepigwa jeki kudhibiti mvua za El-Niño zilizotarajiwa kuanza Oktoba hadi Disemba 2023.

Hatari inayokodolea macho kaunti ndogo tano za Bomet ni mafuriko, maporomoko ya udongo, mashambulio ya radi na kuporomoka kwa machimbo.

Gatuzi hili limeanza mpango wa kutoa hamasa kwa umma kuhusu majanga na jinsi wakazi watajilinda.

“Tumehamasisha kikosi cha wahudumu wa afya, kununua chakula na vifaa vingine pamoja na kuhusisha wanaojitolea kujitokeza ili kusaidia mvua hizi zikianza,” Afisa Mkuu wa Kaunti wa Ugatuzi na Mipango Maalum Eric Cheriyot alisema.

Mvua kubwa za mapema mwaka huu, ziliangusha majengo ya tope huku maji ya yakiporomosha vyoo vya mashimo katika kata za Bingwa na Siongiroi eneobunge la Chepalungu.

Idara ya Kudhibiti Majanga inaamini mipango yake itazuia kutokea tena kwa uharibifu huu.

Familia zinazoishi katika maeneo yaliyo na hatari ya kusombwa na mafuriko, zimetahadharishwa.

Kadhalika, serikali imesihi wakazi kutumia mvua hizi kuwezesha shughuli za kilimo.

  • Tags

You can share this post!

Mhasibu wa KeRRa kujua hatima ya akaunti ya mahari Novemba 9

Kanisa latetea Oburu kushiriki sakramenti

T L