• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Kanisa latetea Oburu kushiriki sakramenti

Kanisa latetea Oburu kushiriki sakramenti

NA JUSTUS OCHIENG

Kwa miaka 80 iliyopita, Seneta wa Siaya Dkt Oburu Oginga hakuwa ametimiza ndoto yake ya kushiriki Sakramenti ya Ushirika Mtakatifu.

Dkt Oburu aliyezaliwa Oktoba 15, 1943, na mvulana wa kwanza wa makamu wa kwanza wa rais Jaramogi Oginga Odinga, alipitia dhiki nyingi, mojawapo ikiwa kunyimwa fursa ya kuidhinishwa na Kanisa la Kianglikana la Kenya (ACK) kushiriki Sakramenti ya Ushirika Mtakatifu.

Dhambi yake, ilikuwa kukosa jina la Kikristo lakini sasa miaka mingi baadaye, Askofu wa Dayosisi ya Bondo amesema alikuwa na zaidi ya mke mmoja, jambo ambalo alisema ni chukizo na sababu ya kunyimwa ushirika huo na Kanisa.

Hata hivyo, Dkt Oginga alipata afueni Jumapili Oktoba 15, 2023 alipoadhimisha miaka 80, wakati Askofu mkuu wa Dayosisi ya Bondo Prof David Kodia, alipokubali kumuidhinisha kupata sakramenti ya Ushirika Mtakatifu.

Lakini hatua hiyo imekashifiwa vikali huku makasisi wakishutumiwa kwa kuenda kinyume na mafundisho ya Kanisa, kwa kuruhusu Dkt Oginga, kaka mkubwa wa kiongozi wa Azimio Raila Odinga, kuthibitishwa kupata sakramenti ya Ushirika Mtakatifu.

“Baadhi ya watu hata walifananisha uthibitisho huo na upendeleo, wakisema alipendelewa kwa sababu ya hadhi yake kama seneta. Baadhi walisema kuna hali nyingi ambazo hazijashughulikiwa na kanisa kwani mtu aliye na wake wengi hapaswi kuruhusiwa kushiriki sakramenti ya Ushirika Mtakatifu,” Prof Kodia aliambia Taifa Leo.

Hata hivyo, askofu huyo ambaye ni mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Makanisa nchini (NCCK), eneo la Nyanza, alikanusha upendeleo wowote, akitetea hatua yake.

“Sheria za kanisa humpa askofu uamuzi wa kuthibitisha au kumrudisha mtu kwenye Ushirika Mtakatifu baada ya kutubu, au kupita wakati fulani,” Prof Kodia alisema.

Akaendelea: “Mheshimiwa Dkt Oburu kamwe hakuchukuliwa hatua zozote za kinidhamu na aliwasilisha ombi lake la kuzingatiwa ili athibitishwe, na askofu baada ya kushauriana na kasisi wa eneo lake alikubali ombi lake na kumthibitisha ipasavyo mchana peupe.”

“Jukumu letu kama Kanisa si kuhukumu bali ni kueneza matendo ya huruma ya Mungu kwa watu wake bila kujali hadhi na hali zao kijamii.”

Viongozi wa kidini wanasema Dkt Oginga aliomba Kanisa kwamba siku yake ya kuadhimisha miaka 80 ya kuzaliwa, iwe ya ” kuzaliwa upya kiroho.”

“Kwa hakika ilimlazimu baba yangu Jaramogi Oginga Odinga kuandika barua kwa makao makuu ya Kanisa la Anglikana Uingereza akilalamikia kukatazwa kwangu kubatizwa kwa kutumia majina ya Kiafrika. Wakati huo, makasisi waliruhusu tu ubatizo wa watoto ambao walikuwa na majina ya Kizungu lakini baba yangu alikataa kunipa jina kama hilo,” seneta huyo anakumbuka.

“Jaramogi alipata jibu kwamba hakuna kinachokataza mtu kubatizwa kwa kutumia jina la Kiafrika na ndipo nilibatizwa. Kwa hivyo imekuwa ngumu kwa muda mrefu kwa sababu tangu wakati huo, nimejaribu kuthibitishwa bila mafanikio.”
Anasema sasa anafuraha kwamba amethibitishwa na amekubaliwa kwa sakramenti.

  • Tags

You can share this post!

Kikosi cha dharura chawekwa Bomet kusubiri mikasa ya El-Nino

DONDOO: Jombi achanganywa na demu mgeni plotini aliyemwomba...

T L